ҽ

Dk.Mpango, makamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dk.Mpango, makamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Makamu Rais wa Tanzania awasihi viongozi wa dini kuungana na serikali kukemea mafundisho yasiyofaa!

Dk.Mpango,Makamu Rais wa Tanzania alitaka Wizara ya Mambo ya Ndani kusimamia kikamilifu Sheria ya Usajili wa Jumuiya pamoja na kanuni zake ili kuhakikisha Taasisi zinazosajiliwa zikiwemo za kidini zinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia malengo na masharti ya usajili wake.Alisema hayo Septemba 7,katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Kanisa la New Life Outreach huko Arusha Tanzania.

Kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais -Tanzania

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaniam Mhesh. Dkt. Philip Mpango alitoa rai kwa viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya, kusimamia kikamilifu Sheria ya Usajili wa Jumuiya pamoja na kanuni zake ili kuhakikisha kuwa Taasisi zinazosajiliwa zikiwemo za kidini zinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia malengo na masharti ya usajili wake. Makamu wa Rais alitoa rai hiyo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Kanisa la New Life Outreach iliyofanyika katika Kanisa hilo Sakina mkoani Arusha. Alisema hivi sasa yameibuka mafundisho ya baadhi ya viongozi wa dini yanayowaaminisha wafuasi wao kutegemea miujiza zaidi ili kupata maendeleo badala ya kufanya kazi kwa bidii.

Ongezeko la wahubiri wanaolimbikiza sadaka kutoka kwa wadhifu

Dkt. Mpango aliongeza kwamba imeshuhudiwa kuongezeka kwa wahubiri wanaojilimbikizia fedha na mali binafsi kutokana na sadaka na mauzo ya vitu mbalimbali na wengi wa wahanga wa mahubiri ya aina hiyo ni wananchi wanaokabiliwa na shida au matatizo mbalimbali ya maisha. Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa dini kuungana na serikali kukemea vikali mafundisho na matendo hayo yasiyofaa katika jamii na yasiyozingatia sheria za nchi. Pia alitoa wito kwa viongozi wote kuwahimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii, maarifa na uzalendo, huku wakimuomba Mwenyezi Mungu abariki kazi zao.

Mmomonyoko wa maadili hasa kwa vijana

Makamu wa Rais halikadhalika alisema kwamba hivi sasa kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii hali inayopelekewa na matumizi holela ya mitandao ya kijamii, ambapo wananchi hususan vijana wengi wanadhani ili kuwa kijana wa kisasa, inawalazimu kuiga mambo yanayooneshwa kwenye mitandao hiyo yakiwemo yale yasiyo endana na mila na desturi. Alisema kukosekana kwa hofu ya Mungu katika jamii kunapelekea kuongezeka kwa matukio ya mauaji ya kikatili, ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto na wanawake, familia za mzazi mmoja, watoto waliozaliwa nje ya ndoa, migogoro ya ndoa, talaka, migogoro ya mirathi na ardhi, ubadhirifu wa mali za umma na matukio ya watu kujinyonga.

Uzembe na kutozingatia sheria barabarani

Dkt. mpango aidha alikemea tabia za uzembe na kutozingatia sheria za usalama barabarani ambazo zimepelekea kushamiri kwa ajali mbaya za barabarani zinazogharimu maisha ya wananchi wengi. Alitoa rai kwa wakaguzi wa magari wa LATRA na Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani kutimiza wajibu wao ili kudhibiti magari mabovu yasiingie barabarani na kuhakikisha vidhibiti mwendo vinafanya kazi, pamoja na kukagua sifa za madereva hasa wa mabasi ya abiria na malori. Aliongeza kwamba wamiliki wa Mabasi na Malori wanapaswa kuhakikisha magari yao yanakuwa na madereva walau 2 kwa safari zote ndefu zinazozidi kilomita 300. Vilevile aliagiza Wakala ya Barabara Nchini (TANROADS) kuhakikisha alama za tahadhari zinawekwa katika maeneo yote hatarishi ya barabara kuu.

Abiria funga mikanda.Toa taarifa kwa kikosi cha usalama barabarani pindi kuna kasi

Makamu, Rais  wa Tanzania alitoa wito kwa wasafiri wote nchini kuzingatia kufunga mikanda wakati wote wa safari na kutoa taarifa kwa Kikosi cha Usalama Barabarani pale dereva wa chombo wanachosafiria anapoendesha kwa mwendo mkali kupita kiasi. Pia Makamu wa Rais aliwasihi viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla kushirikiana na serikali katika kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Alisema uhai wa wanadamu katika dunia unatishiwa na uharibifu wa mazingira ambao umekithiri ambapo pamoja na jitihada mbalimbali za kitaifa na kimataifa zinazochukuliwa kukabiliana na hali hiyo, lakini bado matokeo yake si ya kuridhisha. Aliongeza kwamba uharibifu wa misitu na ukataji wa miti unaonekana katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo mkoani Arusha. Makamu wa Rais alisema Serikali itaendelea kuenzi mchango mkubwa wa madhehebu ya Dini, katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii na itaendelea kusimamia na kulinda haki ya kuabudu kwa wananchi wote kwa mujibu wa ibara ya 19 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwamba wananchi wanaendelea kuishi katika mazingira ya haki na amani.

Mkuu wa Kanisa la New Life Outreach aishukuru Serikali

Kwa upande wake, Muasisi wa Kanisa la New Life Outreach Tanzania Mwinjilisti Dk. Egon Falk aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa kibali cha kuhubiri neno la Mungu kwa miaka 50. Alisema Kanisa hilo litaendelea “kufuata sheria na taratibu za nchi wakati wa utoaji wa huduma ya kuhubiri neno la Mungu na huduma nyingine za kijamii.” Kanisa hilo linamiliki Shule mbili za msingi na moja ya sekondari ambazo zimekuwa zikitoa ufadhili wa masomo kwa watoto wanaopitia mazingira magumu ya Maisha.

Historia ya waanzilishi wa Kanisa la New Life Outreach nchini Tanzania

Egon na Hannah Falk ni familia ambayo ndiyo waanzilishi wa Kanisa la New Life Outreach mnamo mwaka  1974  nchini Tanzania na ambap bado wanaendelea kukuza huduma zao.  Leo hii kuna zaidi ya waajiri 80,  wanaohusika katika Kanisa hilo (NLO.) Hannah alizaliwa na kukulia huko Randers, Jutland nchini Denmark. Alikutana na Egon ambaye alizaliwa na kukulia huko Tejn kwenye kisiwa cha Bornholm kwenye kambi ya vijana kwenye kisiwa cha Bornholm mnamo 1965. Walipendanda sana  na kutambua kwamba Mungu alikuwa amewaleta pamoja kwa kusudi la kueneza habari njema, Injili ya Yesu Kristo. Wamefanya hivyo tangu kuchumbiana kwao mnamo mwaka 1967. Wakiwa wote wainjilisti wamehudumu katika kisiwa cha Bornholm, Norway na katika miji ya Denmark ya Haderslev na Esbjerg. Tangu 1974 wao wamejitolea maisha yao kwa watu wa Tanzania.  Wanafamilia hao wana watoto 3 wazuri. Tina, Ruben na Gitte. Wote wameolewa na wana watoto 8 kati yao wote. Hannah ana jukumu muhimu sana na kubwa katika huduma kama kiongozi wa kila siku. Yeye pia ni mke aliyejitolea na msaidizi wa Egon. Bwana Egon ana huduma ya kuhubiri kwa watu wa Tanzania. Wote hao wakiwa na shauku ya huduma hiyo  hadi watakapofika  kule mbinguni.

Hudumaza  New Life Outreach katika maeneo mengi tofauti

Kwa upande wa elimu Kanisa hili lina Shule kama vile:  Kituo cha watoto yatima, Kanisa, shule ya Biblia na mafunzo ya uongozi, Miradi ya Maji n.k.. Lakini moyo wa Kanisa la New Life Outreach kwa hakika wanabainisha kwamba ni uhamasishaji wa Kiinjili. Kwa upande wao wanalifikia taifa zima la Tanzania kwa ujumbe mzuri wa Yesu Kristo wa: kuaoka,kuombolewa na pepo wabaya na kutoka katika magonjwa mengi ya kiroho."

Dk.Mpango,Makamu Rais wakati wa Jubilei ya Kanisa la New Life Outreach
04 October 2024, 14:59