ĂŰĚŇ˝»ÓŃ

Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari kauli mbiu “Uandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.” Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari kauli mbiu “Uandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.”   (AFP or licensors)

Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, 2024

UNESCO kwa kushirikiana na Shirikisho la Waandishi wa Habari Duniani, IFJ wametoa ripoti yao ikionesha kwamba, katika kipindi cha miaka 15 iliyopita waandishi wa habari 44 waliuawa wakiwa wanachunguza masuala ya mazingira. Kampeni ya Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari ni kwamba kila habari mintarafu mazingira lazima isimuliwe hivyo waandishi wa habari walindwe. Kauli mbiu: "Uandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi"

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Machi inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Uandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.” Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO kwa kushirikiana na Shirikisho la Waandishi wa Habari Duniani, IFJ wametoa ripoti yao ikionesha kwamba, katika kipindi cha miaka 15 iliyopita waandishi wa habari 44 waliuawa wakiwa wanachunguza masuala ya mazingira. Kampeni ya Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari ni kwamba kila habari mintarafu mazingira lazima isimuliwe hivyo waandishi wa habari walindwe. Masuala hayo ni pamoja na jinsi sekta ya madini inavyochafua mazingira, migogoro ya ardhi hasa kwenye maeneo yenye maliasili na bila kusahau changamoto ya watu kukimbia maeneo na nchi zao kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote sanjari na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kipindi hicho cha miaka 15 ni kuanzia mwaka 2009 hadi 2023. Bwana Audrey Azoulay, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, anasema, UNESCO lazima ithibitishe dhamira yake ya kutetea uhuru wa watu kujieleza sanjari na kuwalinda waandishi wa habari popote pale walipo duniani.

Katika Kipindi cha Miaka 15 Waandishi habari 44 wameuwawa
Katika Kipindi cha Miaka 15 Waandishi habari 44 wameuwawa

Wakati huo huo, Bwana Guilherme Canela, Mkuu wa Kitengo cha Uhuru wa Vyombo vya Habari na Usalama wa Waandishi wa Habari, UNESCO amebaini kwamba, kuna waandishi wa habari 44 waliuawa katika kipindi cha miaka 15 iliyopita kwa sababu walikuwa wanaandika habari kuhusu mazingira. Akinukuu ripoti hiyo mpya itokanayo na utafiti uliohusisha waandishi wa habari 905 kutoka nchi 129 zikiwemo za Bara la Afrika, Bwana Canela anasema katika hao 44 waliouawa, ni kesi tano tu ndio wahusika walipatikana na hatia na kuhukumiwa. Asilimia 70% ya waandishi wa habari waliohojiwa walikumbwa na ghasia wakichunguza masuala ya mazingira kama vile uchafuzi utokanao na uchimbaji madini na migogoro ya ardhi. Asilimia 41% kati yao hao walipata mashambulio ya mwilini wengi wao wakiwa wanaume, na kwamba, asilimia 60% walishambuliwa mtandaoni, walengwa wengi wakiwa ni wanawake. Bara la Afrika lilibeba theluthi mbili ya matukio ya mashambulizi ya mwilini.

UNESCO imedhamiria kuwalinda na kuwatetea waandishi wa habari
UNESCO imedhamiria kuwalinda na kuwatetea waandishi wa habari

Kama hiyo haitoshi, asilimia 25% walikabiliwa na kesi za madai kwa lengo la kuwanyamazisha. Bwana Canela amesema “tuligundua pia matukio 749 katika nchi 89 ya mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari au vyombo vya habari kwa sababu tu ya kuripoti masuala ya uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Na kwa bahati mbaya watekelezaji wakuu wa vitendo hivi vya mashambulizi walikuwa ni watu kutoka Serikalini yaani: Polisi, wanasiasa au watu wenye uhusiano na serikali kwa njia moja au nyingine.” Hata wakati wa maandamano waandishi wa habari walilengwa kwani ripoti hiyo ya kurasa 18 inasema katika kipindi hicho cha miaka 15 kuanzia mwaka 2019 hadi 2023, waandishi wa habari 194 walishambuliwa na matukio mengi ni Barani Ulaya, Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kusini na kwenye Visiwa Visiwa vya Karibi (na kwa Lugha ya Kiingereza Caribbean.) Hivyo UNESCO inatoa wito kwamba “katika siku hii ya uhuru wa vyombo vya habari kwa mwaka huu wa 2024 kuna haja kusisitiza umuhimu wa ulinzi kwa waandishi wa habari wanaoripoti kuhusu masuala ya mazingira nyumba ya wote, kwa sababu kama si hivyo, Jumuiya ya Kimataifa itakuwa na maeneo ya ukimya, ambako huko wanajamii hawafahamu au hawajapatiwa taarifa kwa njia isiyoegemea upande wowote juu ya kile kinachoendelea kuhusiana na aina hizi za mivutano na kinzani.

Uhuru wa vyombo vya habari
03 May 2024, 15:53