ҽ

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, akamilishe uchunguzi kwenye wizi wa kimtandao Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, akamilishe uchunguzi kwenye wizi wa kimtandao  (ANSA)

Wizi wa Fedha Umekithiri Katika Miradi ya Umma Tanzania

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kasssim Majaliwa aagiza TAKUKURU ichunguze ubadhirifu wa fedha ya Umma Bunda Vijijini. Kwa hakika wizi na ubadhirifu wa mali ya umma vimekithiri na kwamba Serikali inaendelea na uratibu wa mpango wa kuwa na viwanda vya mazao ya mifugo.Majaliwa amewataka Watanzania kuwa walinzi wa miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ili iweze kukamilika kwa wakati na kutoa huduma kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Bunda, Mkoani Mara.

unaotumika katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, akamilishe uchunguzi kwenye wizi wa kimtandao. “Kamanda wa TAKUKURU Mkoa fuatilia hili suala kwa haraka, najua mna tabia ya kufanya uchunguzi wenu kwa muda mrefu. Nataka hili likamilike kwa haraka kwa sababu nilishatuma timu yangu na kazi kubwa imeshafanyika.” Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jioni Jumatatu, Februari 26, 2024 wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda pamoja na wale wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda uliofanyika kwenye ukumbi wa Herieth, wilayani Bunda mkoani Mara. Akizungumza na watumishi hao, Waziri Mkuu amesema Serikali ina utaratibu wa kukamilisha matumizi ya fedha zilizopangwa ifikapo Juni 30, kila mwaka. “Ikifika wakati huo, HAZINA wana uwezo wa kuichukua na ikabaki labda iwe imeandikwa barua ya kuombewa kibali maalum cha kuhamisha fedha kwenda mwaka unaofuata.” “Hapa Bunda mnatumia mwanya huo, kuziombea kibali. Kisha zinahamishiwa kwenye akaunti jumuifu ya amana, halafu zinatolewa na kutumiwa kinyume na utaratibu.” Amesema mchezo huo unafanywa na watu wachache kwenye Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na watumishi wasio waaminifu wa kitengo cha akaunti jumuifu ya amana kilichopo OR-TAMISEMI na hata Katibu Mkuu hawezi kujua mchezo huo wala Madiwani pia hawawezi kujua. “Mara nyingi wanaocheza mchezo huo hapa Bunda, ni Mkurugenzi wa Halmashauri, Mweka Hazina na Mkurugenzi wa Mipango wa Halmashauri. Kwa mfano, mwaka wa fedha 2021/2022 waliomba kibali cha kuhamisha sh. milioni 871.4 ili ziweze kutumika baada ya muda. Lakini walihamisha sh. milioni 962 na kuzihifadhi huko.”

Rais Samia Suluhu Hassan anawapenda na kuwathamini watanzania wote
Rais Samia Suluhu Hassan anawapenda na kuwathamini watanzania wote

“Mbali na hizo, kupitia mawasiliano baina ya hawa watatu na wenzao wa TAMISEMI, zikaingizwa tena sh. milioni 215.3. Je, ninyi Waheshimiwa Madiwani mliziomba hizo fedha? Je mlijulishwa kwamba kuna fedha za ziada zimeombwa?” alihoji Waziri Mkuu na kujibiwa hapana na madiwani waliokuwepo. Waziri Mkuu amesema kibaya zaidi, fedha hizo zinapotoka, zinaelekezwa kwenye kazi ambazo tayari zilishatengewa vifungu na ambazo tayari ziliombewa kibali. “Walitoa fedha na kuandika zimetumika kwenye jengo la utawala, kutengeneza fedha za hesabu za mwaka, jengo la wagonjwa wa dharura, posho ya kujikimu ya walimu wapya wa shule za msingi. Hizi zote zilikuwa na fedha zake, Je, zimeenda wapi?” “Kamanda wa TAKUKURU, nataka ufuatilie ni nani aliomba hizo sh. milioni 215.3? Ni kwa nini fedha hizi zitumike kwenye kazi ambazo tayari zina mafungu yake? Je, ni kweli hawa walimu walilipwa hizo posho? Kwa nini madiwani hawakujulishwa kuhusu mchakato wa fedha hizi?” Waziri Mkuu anaendelea za ziara yake mkoani Mara kwa kuhutubia wakazi wa Mji wa Bunda. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekemea vitendo vya wizi na uzembe kwenye usimamizi wa ujenzi wa miradi ya umma nchini. “Tumeshaibiwa mifuko zaidi ya 600 kwenye ujenzi wa shule hii ya sekondari ya wasichana ya Mara, hakuna usimamizi, hakuna anayejali, mngeanza kuchukua hatua ninyi wenyewe Halmashauri kabla hata Mkuu wa Mkoa hajaja” Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Februari 26, 2026 alipokagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mara kata ya Buramba wilaya ya Bunda mkoani Mara. “Kwanini Muentertain wizi? Watu wanaiba mara ya kwanza, mara ya pili mmeshindwa kuchukua hatua za kuwadhibiti wasirudie tena? Halafu si hapa tuu, hata hospitali ya wilaya ina matatizo mengi, mmeshang’oa na milango iliyofungwa, mmeshaiba na vifaa tiba ikiwemo mashine ya X-Ray, sasa nyie Bunda mkoje?” Alihoji Mheshimiwa Majaliwa.

Wananchi wawe walinzi na wasimamizi wa miradi ya umma.
Wananchi wawe walinzi na wasimamizi wa miradi ya umma.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa haridhishwi na utendaji kazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa kukosa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo. Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Bunda Dkt. Vicent Naano adhibiti vitendo vya wizi kwenye Halmashauri hiyo. “Halmashauri hii fedha za Serikali zinakuja nyingi sana, na si lazima aje Mkuu wa Mkoa, wewe una Kamati ya Usalama, uzembe ni mwingi, hatuwezi kukubaliana nalo hili.” Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Watanzania kuwa walinzi wa miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ili iweze kukamilika kwa wakati na kutoa huduma kama ilivyokusudiwa na Rais Dkt. Samia. “Wananchi ni muhimu kutoa taarifa ili kuzilinda rasilimali fedha na miradi, iwe ya shule, afya, elimu hata barabara hili pia ni jukumu lenu, mkiona dalili za wizi kwenye miradi yetu toeni taarifa, hatuwezi kuwavumilia wezi hawa, wanakwamisha juhudi za Rais wetu kuleta maendeleo.” Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mara, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wajenzi wa shule hiyo kufanya kazi usiku na mchana ili iweze kukamilika ifikapo Julai 2024 na ianze kupokea wanafunzi. Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inawapenda Watanzania ndiyo maana inatekeleza miradi mingi na kutoa wataalamu katika nyanja zote ili waweze kuwahudumia wananchi.

Wizi umekithiri katika miradi ya umma nchini Tanzania
Wizi umekithiri katika miradi ya umma nchini Tanzania

“Serikali ya awamu ya sita inawapenda Watanzania wote ndiyo maana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anatekeleza miradi mbalimbali ya maeneo katika sekta zote za maendeleo kuanzia ngazi ya Taifa hadi vijijini.” Waziri Mkuu ameyasema hayo Jumatatu, Februari 26, 2024 wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa maeneo ya Mariwanda na Sabasita, wilayani Bunda akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku tano mkoani Mara. Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni imara na ina nia ya dhati ya kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa kufikisha maendeleo kwenye sekta zote za huduma za jamii katika kila eneo nchini. Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa shule ya msingi Sabasita, Mheshimiwa Majaliwa amesema mkakati wa Serikali ni kujenga shule kwenye kila kijiji na kama kuna vitongoji vikubwa au kuna kijiji kina watu wengi, mpango uwe ni kuongeza shule. Shule hiyo ambayo imejengwa maalum chini ya mpango wa BOOST ili kuwasaidia watoto wa wafugaji wasitembee umbali mrefu kupata elimu, imegharimu sh. milioni 348.2 ambazo zimejenga madarasa tisa yakiwemo saba ya elimu ya msingi na mawili ya elimu ya awali. Kabla shule hiyo haijajengwa, watoto walikuwa wakitembea umbali wa km. tano na sasa umbali huo hauzidi km. moja.

Ujenzi wa Shule ya Wasichana Mara ukamilike Julai 2024
Ujenzi wa Shule ya Wasichana Mara ukamilike Julai 2024

Fedha hizo pia zimetumika kujenga jengo la utawala, matundu ya vyoo 16 ambapo nane ni vya shule ya msingi, sita ni ya awali na mawili ni ya walimu. Ujenzi wa shule hiyo ulianza Mei 16, 2023 na ulikamilika Julai 30, 2023. Akiwa njiani kuelekea Sabasita, Waziri Mkuu alisimama Mariwanda na kuwasalimia wananchi waliojitokeza njiani kumpokea na kuwaeleza kuwa Serikali inaendelea na uratibu wa mpango wa kuwa na viwanda vya mazao ya mifugo. “Mifugo ni maisha, mifugo ni uchumi, mifugo ni uwezeshaji wa mtu binafsi ndiyo maana Serikali inawaletea maafisa ugani ili wawasaidie kwenye sekta hiyo. Endeleeni kufuga na mzingatie masharti ya ufugaji ili muweze kukuza uchumi wenu,” amesisitiza. Waziri Mkuu alimwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt. Zablon Masatu akae na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt. Adinani Hamidu ili waangalie uwezekano wa kuongeza vigezo kwenye zahanati ya kijiji kwa kuongeza majengo ya kuhudumia mama na mtoto kutokana na idadi kubwa ya wakazi kwenye kijiji hicho. Akiwa kata ya Buramba katika jimbo la Mwibara, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mkoa wa Mara ambayo inatarajiwa kugharimu sh. bilioni 4 na itakapokamilika, itachukua wanafunzi wa kike kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita. Shule ambayo pia itakuwa ya bweni, ilipokea sh. bilioni 3 na hadi sasa imekwishagharimu sh. bilioni 2.82 na kuna baki ya sh. milioni 176.7. Waziri Mkuu aliwasisitiza viongozi wa Halmashauri ya Bunda wasimamie mradi huo na mafundi ujenzi wa shule hiyo wafanye kazi usiku na mchana ili ukamilike mapema na ifikapo Julai, mwaka huu wanafunzi wa kidato cha tano waanze masomo.

27 February 2024, 09:58