ҽ

Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Walinzi wa Papa Kutoka Uswis Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Walinzi wa Papa Kutoka Uswis   (Vatican Media)

Mfuko wa Walinzi wa Papa Kutoka Uswiss: Huduma Kwa Mafao ya Wengi

Papa Francisko asema: Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Walinzi wa Papa Kutoka Uswis “Fondazione della Guardia Svizzera Pontificia,” yanafanyika wakati huu wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, kwa kufanya hija ya matumaini kwenye Makaburi ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani. Hii ni fursa kwa wajumbe wa Mfuko huu, kuweza kupyaisha tena imani yao kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kikosi cha Walinzi wa Papa kutoka Uswisi, kilichoundwa kunako mwaka 1506 na Papa Giulio II, maarufu kama “Swiss Guards” kina dhamana na utume unaojikita katika wito, uaminifu, umakini na sadaka inayotekelezwa kwa moyo wa unyenyekevu pasi na makuu. Kikosi hiki kilianzishwa na Papa Giulio II kunako tarehe 22 Januari 1506. Ni katika muktadha huu, kunako mwaka 2000 ya Ukristo, chini ya uongozi wa Mtakatifu Yohane Paulo II, Mfuko wa Walinzi wa Papa kutoka Uswis uliundwa na kwa Mwaka 2025, Mfuko unaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, sanjari na Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa matumaini.” Matumaini ya waamini yametundikwa juu ya Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu.

Jubilei ya Miaka 25 ya Mfufuko wa Walinzi wa Papa 2000-2025
Jubilei ya Miaka 25 ya Mfufuko wa Walinzi wa Papa 2000-2025

Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Walinzi wa Papa Kutoka Uswis “Fondazione della Guardia Svizzera Pontificia,” yanafanyika wakati huu wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, kwa kufanya hija ya matumaini kwenye Makaburi ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani. Hii ni fursa kwa wajumbe wa Mfuko huu, kuweza kupyaisha tena imani yao kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huyu ni Mwana wa Mungu aliye hai. Dhamana na utume wao, unafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika ari na moyo wa imani na mapendo, tayari kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na majukumu yake kwa Kanisa la Kiulimwengu. Baba Mtakatifu Francisko amependa kuchukua fursa hii kuwashukuru kwa dhamana na utume wao, kwani ameshuhudia yote haya kwa macho yake binafsi.

Kikosi cha Ulinzi wa Papa Kutoka Uswis kilianzishwa mwaka 1506
Kikosi cha Ulinzi wa Papa Kutoka Uswis kilianzishwa mwaka 1506

Hii ni huduma inayotekelezwa kwa ari na moyo mkuu pamoja na uaminifu. Walinzi hawa wamekuwa mstari wa mbele kuwapokea na kuwakaribisha “mahujaji wa matumaini” wanaotembelea mjini Vatican. Kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika maisha na historia ya walinzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, lakini jambo la msingi ni ulinzi kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, pamoja na kuwakaribisha na kuwapokea mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaofika mjini Vatican kusali pamoja na kuonana na Baba Mtakatifu. Hii ni huduma inayohitaji uvumilivu pamoja na heshima kwa watu na mali zao. Huu ni Mfuko ambao umekuwa mstari wa mbele kuwahudumia walinzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kuchangia: Ustawi na maendeleo ya familia ya Askari hawa; kugharimia elimu na majiundo yao; kusomesha watoto wao katika shule na taasisi kwa watu husika. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kuona kwamba, Walinzi wa Papa kutoka Uswis wanaoa, ili hatimaye waweze kuwa na watoto, ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Kwa hakika watasaidia kuongeza idadi ya watoto wa Mungu, ustawi, maendeleo na mafao ya familia; jambo msingi kwa Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Huduma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Huduma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii pia kuwashukuru Askari wote wanaomaliza muda wao wa huduma na kurejea nyumbani kwao na kwamba, kuna baadhi yao ambao wameendeleza mawasiliano mema kwa njia ya simu, kwa kumtembelea wanapokuwa mjini Roma au kumkumbuka kwa zawadi mbalimbali. Mambo yote haya ni mazuri ili kuwawezesha Askari hawa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa amani na utulivu wa ndani; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ushirikiano na mshikamano kati ya Walinzi wa Papa pamoja na Mfuko wa Walinzi wa Papa Kutoka Uswis “Fondazione della Guardia Svizzera Pontificia,” unaonesha kwamba, Taasisi hizi mbili zinashirikiana kwa karibu sana, mwaliko kwa nwatu wa Mungu kuendelea kushikamana katika umoja. Baba Mtakatifu amewashukuru wajumbe Mfuko wa Walinzi wa Papa Kutoka Uswis “Fondazione della Guardia Svizzera Pontificia,” kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwao!

Mfuko wa Walinzi wa Papa
19 January 2025, 11:41