Papa:sote tukatae mantiki za vurugu,tushirikiane kwa manufaa ya wote!
Pope
Baba Mtakatifu Francisko akikutana alhamisi asubuhi tarehe 16 Januari 2025 katika Ukumbi wa Maktaba ya Jumba la Kitume mjini Vatican na wajumbe kutoka Albania wakiongozwa na Haxhi Baba Edmond Brahimaj, kiongozi wa Waislamu wa Bektashi wa Tirana, aliwakaribisha na kushukuru hata Baraza la kipapa la Mazungumzo ya Kidini kufanikisha mkutano huo. Kila mara viongozi wa kidini wanapokutana pamoja kwa moyo wa kuheshimiana na kujitolea kwa utamaduni wa kukutana, kwa njia ya mazungumzo, maelewano na ushirikiano, tumaini letu la kuwa na ulimwengu ulio bora na wenye haki zaidi linafanywa upya na kuthibitishwa. Wakati wetu unahitaji tumaini kama hilo!” Papa alisisitiza.
Papa alikazia kusema kuwa “Uhusiano wa kirafiki kati ya Kanisa Katoliki, Albania na Jumuiya ya Bektashi ni mzuri kwetu sote, na nina hakika kwamba vifungo hivi vitaimarishwa zaidi katika huduma ya udugu na kuishi pamoja kwa amani kati ya watu.” Papa akitazama pepo za vita na vurugu alisema “Katika nyakati hizi ngumu, sote tunaitwa kukataa mantiki ya vurugu na mifarakano, kukumbatia ile ya kukutana, urafiki na ushirikiano katika kutafuta manufaa ya wote. Kwa hakika, imani zetu za kidini hutusaidia kukumbatia kwa uwazi zaidi tunu hizi za kimsingi, zinazofaa kwa ubinadamu wetu wa kawaida, "kuruhusu sauti tofauti kwa pamoja kuunda wimbo mzuri na wenye upatanisho" (Fratelli tutti, 283).
Katika suala hilo Papa anafikiria kwa shukrani kwa nyakati nyingi za kukutana kidugu ambazo zimetokea kati ya jumuiya ya Bektashi na Kanisa Katoliki, kama vile Sala ya Amani katika Balkan mwaka 1993 na Siku ya Dunia ya Kuombea Amani huko Assisi 2011.” Uzinduzi wa Hekalu la Bektashi huko Tirana, mwaka wa 2015, ulikuwa wakati mzuri sana wa ukaribu na urafiki. Kwa njia hiyo ni matumaini ya Papa “kwamba Jumuiya ya Bektashi, pamoja na Waislamu wengine, Wakristo na waamini wengine wote waliopo Albania, wanaweza kutumika kama daraja la upatanisho na kutajirishana si tu ndani ya nchi yao tu, bali pia kati ya Mashariki na Magharibi. Licha ya changamoto za sasa, mazungumzo baina ya dini yana nafasi ya pekee katika kujenga mustakabali wa upatanisho, haki na amani ambayo watu wa dunia na hasa vijana wanatamani kwa dhati.” Papa amehitimisha kwa kuwakikisha, maombi yake na baraka zake kwa kazi yao muhimu na kwa watu wote wapendwa wa Albania. Na pia amewaomba,wamuombee.