Papa katika jamii zetu,kuna njia nyingi za kunyanyaswa na kuteswa watoto!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumatato tarehe 15 Januari 2025 aliendeleza mzunguko mpya wa Katekesi kwa mada ya : Anayependwa zaidi na Baba. Kabla ya katekesi imesomwa Injili ya Mt 18,1-3.6: Wakati huo wanafunzi walimwendea Yesu wakasema, Ni nani aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Kisha akamwita mtoto mdogo, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipogeuka na kuwa kama watoto wadogo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. […] Yeyote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, ingekuwa afadhali afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia na kutoswa katika kilindi cha bahari.”
Baba Mtakatifu Francisko ameanza kusema kuwa katika katekesi ilyopita tulizungumza kuhusu watoto, na leo tutazungumza kuhusu watoto pia. Juma lililopita tuliakisi jinsi gani katika kazi yake, Yesu alizungumza mara kwa mara juu ya umuhimu wa kuwalinda, kuwakaribisha na kuwapenda watoto wadogo. Hata hivyo, leo hii katika ulimwengu, mamia ya mamilioni ya watoto, ingawa si wa umri wa unaostahili kabisa wa kutimiza wajibu wa utu uzima, wanalazimishwa kufanya kazi na wengi wao wanakabiliwa na kazi hatari sana. Bila kusahau watoto wanaosafirishwa kwa ukahaba au picha mbaya na ndoa za kulazimishwa. Na hiyo ni uchungu kidogo. Katika jamii zetu, kwa bahati mbaya, kuna njia nyingi ambazo watoto wananyanyaswa na kuteswa. Unyanyasaji wa watoto, wa asili yoyote, ni kitendo cha kudharauliwa na, ni kitendo kibaya. Sio tauni tu kwa jamii, hapana, ni uhalifu! Huu ni uvunjaji mkubwa sana wa amri za Mungu. Hata kesi moja tayari ni nyingi sana.
Papa alisema kwa hiyo ni lazima kuamsha dhamiri zetu, kufanya ukaribu na mshikamano thabiti na watoto na vijana walionyanyaswa, na wakati huo huo kujenga uaminifu na ushirikiano kati ya wale ambao wamejitolea kuwapa fursa na maeneo salama ya kukua kwa amani. Papa ametoa mfano mmoja kuwa “Ninajua nchi katika Amerika ya Kusini ambapo tunda maalum, sana hukua, liitwalo arandano [aina ya blueberry]. Ili kuvuna matunda yake inahitaji mikono minyororo na wanaofanya kazi ni watoto, wanawafanya watumwa katika mavuno.” Umaskini ulioenea, ukosefu wa zana za kijamii za kusaidia familia, kuongezeka kwa kutengwa katika miaka ya hivi karibuni pamoja na ukosefu wa ajira na usalama wa kazi ni mambo ambayo yanapunguza bei ya juu zaidi ya kulipa kwa vijana zaidi. Katika miji mikuu, ambapo migawanyiko ya kijamii na uharibifu wa maadili "unaumana", kuna watoto walioajiriwa katika uuzaji wa dawa za kulevya na shughuli nyingi tofauti haramu. Ni watoto wangapi kati ya hawa ambao tumewaona wakianguka kama waathiriwa wa sadaka! Wakati mwingine cha kusikitisha wanashawishiwa kuwa "wauaji wa wenzao na pia kujidhuru wenyewe, utu wao na ubinadamu. Na bado, wakati mwingine barabarani, katika vitongoji vya parokia, maisha haya yaliyopotea yanajitokeza machoni petu, mara nyingi tunaangalia upande mwingine.
Papa Fracisko amesisitiza kuwa “Kuna kesi katika nchi yangu pia, mvulana anayeitwa Loan mnajua vizuri. Hii imefanyika! Papa amekazia kusema. Wengine wanarudi na makovu, wengine wanakufa. Kwa sababu hiyo Papa amependa kumkumbuka kijana huyo Loan. Ni vigumu kwetu kukiri dhuluma ya kijamii ambayo inasukuma watoto wawili, labda wenyeji wa kitongoji kimoja au jengo la ghorofa, kuchukua njia na hatima zinazopingana, kwa sababu mmoja wa hao wawili alizaliwa katika familia duni. Mgawanyiko usiokubalika wa kibinadamu na kijamii: kati ya wale wanaoweza kuota na wale ambao lazima washindwe kuota ndoto. Lakini Yesu anataka sisi sote tuwe huru na wenye furaha; na kama anapenda kila mwanamume na kila mwanamke kama mwanawe na binti yake, anawapenda wadogo kwa upole wote wa moyo wake. Kwa hiyo anatuomba tusimame na kusikiliza mateso ya wale wasio na sauti, ya wale ambao hawana elimu.
Kupambana na vita vya unyonyaji hasa unyonyaji wa watoto ndio njia kuu ya kujenga mustakabali mwema wa jamii kwa ujumla. “Baadhi ya nchi zimekuwa na hekima ya kuandika haki za watoto. Watoto wana haki. Tutazame kwenye mtandao wenyewe jii ya haki za watoto ni nini," Papa alishauri. Kwa hiyo tunaweza kujiuliza: je ninaweza kufanya nini? Kwanza kabisa, tunapaswa kutambua kwamba ikiwa tunataka kutokomeza utumikishwaji wa watoto, hatuwezi kuwa washiriki katika hilo. Na sisi ni lini? Kwa mfano tunaponunua bidhaa zinazotumia ajira ya watoto. Ninawezaje kula na kuvaa nikijua kwamba nyuma ya chakula hicho au nguo hizo kuna watoto walionyonywa, wanaofanya kazi badala ya kwenda shule? Ufahamu wa kile tunachonunua ni hatua ya kwanza ili kuepuka kuwa washiriki. Tutazame bidhaa hizo zinatoka wapi, Papa Francisko ameshauri.
Papa hata hivyo alikazia kusema "Wengine watasema kwamba, kama watu binafsi, hatuwezi kufanya mengi. Ni kweli, lakini kila mmoja wetu anaweza kuwa tone ambalo, pamoja na matone mengine mengi, linaweza kuwa bahari. Hata hivyo, ni muhimu pia kuzikumbusha taasisi, zikiwemo za kikanisa, na biashara juu ya wajibu wao: wanaweza kuleta mabadiliko kwa kuhamisha uwekezaji wao kuelekea makampuni ambayo hayatumii au kuruhusu ajira za watoto. Mataifa mengi na Mashirika ya Kimataifa tayari yametunga sheria na maagizo dhidi ya ajira za watoto, lakini mengi zaidi yanaweza kufanywa. Papa Francisko ameongeza kusema “Pia ninawaomba waandishi wa habari - kuna baadhi ya waandishi wa habari hapa - kufanya sehemu yao: wanaweza kusaidia kuongeza ufahamu wa tatizo na kusaidia kutafuta ufumbuzi. Msiogope, kutoa ripoti, yaani ripoti mambo haya.”
“Na ninawashukuru wale wote ambao hawageuzi visogo wanapoona watoto wanalazimishwa kuwa watu wazima haraka sana. Daima tukumbuke maneno ya Yesu: “Yoyote mliyomtendea mmoja wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi” (Mt 25:40).” Mtakatifu Teresa wa Calcutta, mfanyakazi mwenye furaha katika shamba la mizabibu la Bwana, alikuwa mama wa watoto wasio na uwezo na waliosahaulika. Kwa wororo na uangalifu wa macho yake, anaweza kutusindikiza nasi ili kuwaona watoto wadogo wasioonekana, watumwa wengi sana wa ulimwengu ambao hatuwezi kuacha udhalimu wake. Kwa sababu furaha ya wanyonge hujenga amani kwa wote. Papa Francisko kwa kuhitimisha na moja ya sala ya Mtakatifu wa maskini kwamba: "Na kwa Mama Teresa tunatoa sauti kwa ajili ya watoto: "Ninaomba mahali salama, mMahali ambapo ninaweza kucheza, ninaomba tabasamu la yule anayejua kupenda. Ninaomba haki ya kuwa mtoto, ya kuwa tumaini la ulimwengu bora. Ninaomba niweze kukua kama mtu. Je ninaweza kukutegemea wewe?(Mt. Teresa wa Calcutta), alihitimisha Papa Francisko.