ҽ

Juma la 58 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2024 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, linanogeshwa na kauli mbiu “Je, unayasadiki hayo?” Yn 11:26 Juma la 58 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2024 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, linanogeshwa na kauli mbiu “Je, unayasadiki hayo?” Yn 11:26   (Vatican Media)

Maadhimisho ya Juma la 58 La Kuombea Umoja Wa Wakristo 2025: Kanuni ya Imani

Juma la 58 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2024 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, linanogeshwa na kauli mbiu “Je, unayasadiki hayo?” Yn 11:26 Tafakari ya Mwaka huu inajikita zaidi katika Kanuni ya Imani ya Nicea, ambayo kwa Mwaka 2025, Kanisa linaadhimisha kumbukizi ya Miaka 1700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipofanyika kunako mwaka 325! Kanuni ya Imani ya NICEA Muhimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Mwaka huu Wakristo wote wanaadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake. Kanuni ya Imani ya Nicea-Constantinopoli ni formula rasmi ambayo ilipitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Kwanza wa Nicea (325) ikakamilishwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) ili kubainisha imani sahihi ya Kanisa Katoliki dhidi ya uzushi, hasa wa Ario na wafuasi wake. Katika mazingira hayo, lengo kuu lilikuwa kwanza kabisa ni kumkiri Kristo Yesu “Mungu kweli kwa Mungu kweli” yaani Mungu kweli sawa na Baba, halafu kwamba Roho Mtakatifu anastahili kuabudiwa pamoja na Baba na Mwana (Utatu Mtakatifu). Wakristo wanataka kutembea pamoja na Kristo ambaye ni njia, ukweli na uzima. Watu wanamtafuta Kristo Yesu hata bila ya kutambua. Fumbo la Pasaka, linaonesha kwa namna ya pekee, utukufu wa Kristo Yesu kati ya watu wake hadi pale atakapokuja tena kuwahukumu wazima na wafu. Katika hija ya maisha ya kila siku, waamini wanajitahidi kumwilisha Fumbo la Ukombozi, kiini cha maadhimisho haya ni Liturujia ya Mwaka wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, Sikukuu tatu zinazoonesha: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, yaani Sherehe ya Pasaka ambayo kwa Mwaka huu itaadhimishwa hapo tarehe 20 Aprili 2025. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hata Mwaka 2025 Mama Kanisa anawaalika watoto wake kusali ili kuombea umoja wa Wakristo na hatimaye kujenga familia kubwa na kuendelea kutekeleza mapenzi ya Kristo Yesu anayewataka wafuasi wake “Wote wawe na umoja.” Yn 17:21.

Kauli mbiu "Je, unayasadiki hayo?
Kauli mbiu "Je, unayasadiki hayo?

Kumbe, Juma la 58 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2024 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, linanogeshwa na kauli mbiu “Je, unayasadiki hayo?” Yn 11:26 Tafakari ya Mwaka huu inajikita zaidi katika Kanuni ya Imani ya Nicea, ambayo kwa Mwaka 2025, Kanisa linaadhimisha kumbukizi ya Miaka 1700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipofanyika kunako mwaka 325. Mwaka huu, Wakristo wanataka kushuhudia na kuungama tena imani moja. Hii ni fursa na changamoto katika majadiliano ya kiekumene katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika, tarehe 19 Januari 2025 amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo, ili wapate kutoka kwa Mungu zawadi ya thamani kubwa ya ushirika kamili kati ya wanafunzi wa Kristo Yesu.

Sala ya Kristo "Ili wote wawe na umoja."
Sala ya Kristo "Ili wote wawe na umoja."

KANUNI YA IMANI: Nasadiki kwa Mungu mmoja Baba mwenyezi, Muumba wa mbingu na dunia na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Nasadiki kwa Bwana mmoja, Yesu Kristo, Mwanae pekee wa Mungu, aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli, aliyezaliwa, bila kuumbwa, mwenye umungu mmoja na Baba: ambaye vitu vyote vimeumbwa naye. Alishuka kutoka mbinguni, kwa ajili yetu sisi wanadamu, na kwa ajili ya wokovu wetu. Akatwaa mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria, akawa mwanadamu. Akasulubiwa kwa ajili yetu sisi, kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato; akateswa, akafa, akazikwa, siku ya tatu akafufuka, kadiri ya Maandiko, akapaa mbinguni, amekaa kuume kwa Baba. Atakuja tena kwa utukufu, kuwahukumu wazima na wafu, nao ufalme wake hautakuwa na mwisho. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa, pamoja na Baba na Mwana: aliyenena kwa vinywa vya manabii. Nasadiki kwa Kanisa moja, takatifu, katoliki, la Mitume. Naungama ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi. Nangojea na ufufuko wa wafu, na uzima wa milele ijayo. Amina. Kumbe, Kristo Yesu ndiye kiini cha tasahufi ya majadiliano ya kiekumene. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican wanasema Wakristo wote wanawajibika kushiriki katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kufikia umoja kamili na timilifu mintarafu fadhila za Kimungu katika Biblia na Liturujia, Mahubiri ya Neno la Mungu na Katekesi, Utume wa waamini walei, mtindo wa maisha ya kitawa na maisha ya kiroho katika ndoa; mambo yote haya ni muhimu katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Hakuna uekumene wa kweli pasi na toba na wongofu wa kweli; sadaka na upendo kwa jirani na hatimaye, ni fadhila ya unyenyekevu. Dhambi dhidi ya umoja wa Wakristo inaendelea kuwatafuna taratibu. Waamini wakumbuke kwamba, kadiri watakavyo jitahidi kuishi matakatifu, kufuatana na tunu za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile, watahamasishwa na watatekeleza umoja wa Wakristo, ikiwa kama wameungana na Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Juma la 58 la Kuombea Umoja wa Wakristo 2025
Juma la 58 la Kuombea Umoja wa Wakristo 2025

Kumbukizi ya Miaka 1700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipofanyika kunako mwaka 325 ni mwaliko kwa Makanisa na Jumuiya za Kikristo kugundua tena umuhimu wa Kanuni ya Imani, tayari kupyaisha imani yao kwa Kristo Yesu, tayari kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoibuka kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; Kristo Yesu mwenye Umungu mmoja sawa na Baba. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kutafuta tarehe moja, watakayoadhimisha Pasaka ya Bwana. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inapewa kipaumbele cha pekee katika majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa mengine hali inayojionesha katika ngazi kuu tatu; Kanisa mahalia, Kanisa la Kikanda na Kanisa la Kiulimwengu. Hapa mkazo ni kuhusu umoja wa Kanisa ndio changamoto kubwa inayopewa kipaumbele cha kwanza kama ilivyojionesha kwenye Tamko la Ravenna la Mwaka 2007. Tamko hili linagusia umuhimu wa huduma kwa watu wa Mungu.

Mtaguso wa NICEA, Jubilei ya Miaka 1700
Mtaguso wa NICEA, Jubilei ya Miaka 1700

Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema, kuna haja ya kufanya upatanisho wa kiekumene kati ya dhana ya Sinodi na Maisha ya Mkuu wa Kanisa. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki bado ni changa sana ikilinganishwa na Waorthodox. Inawezakana kabisa kutambua dhamana na nafasi ya viongozi wakuu wa Makanisa. Maamuzi yaliyofanywa na Mtaguso wa NICEA wa Mwaka 325 na Mtaguzo wa Calcedonia wa Mwaka 541 ni muhimu sana katika masuala ya uongozi wa Kanisa kwa kutambua kati ya Maaskofu ni nani kiongozi wao mkuu, ili Mwenyezi Mungu aweze kutukuzwa na mwanadamu kutakatifuzwa kwa njia ya Roho Mtakatifu. Dhana ya Sinodi inasimikwa katika muktadha wa kutembea kwa pamoja na kusikilizana na hivyo, Makanisa kuendelea kutajirishana kwani Sinodi ni mchakato unaofumbatwa katika majadiliano ya kiekumene. Baada ya maadhimisho ya Mtaguso wa NICEA, hali ya hewa kisiasa ilichafuka. Mahusiano na mafungamano kati ya Kanisa na Serikali yakaingia dosari. Hili ni jambo ambalo pia linapaswa kufanyiwa tafakari ya kina, ili kuboresha mahusiano kati ya Kanisa na Serikali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Kumbe, kumbukizi ya Miaka 1,700 tangu kuadhimishwa Mtaguso wa NICEA ni fursa ya kupyaisha imani, ushirika wa kiekumene, ungamo la imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; Mungu kutoka kwa Mungu kweli, mwanga kwa mwanga, mwenye umungu mmoja sawa na Baba. Ni wakati wa kuangalia changamoto za Mama Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Umoja wa Wakristo
19 January 2025, 15:16