ҽ

Baba Mtakatifu anasema maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa matumaini.” Baba Mtakatifu anasema maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa matumaini.”   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kongamano la Kitume: Kumtangaza na Kumshuhudia Kristo Yesu Kwa Njia ya Maisha Adili

Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza kwa uaminifu wao kwa Injili chemchemi na mwanga wa matumaini, Kristo Yesu ni tumaini la waja wake, lango la matumaini, chemchemi ya Habari Njema ya Wokovu. Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili mwaliko kwa waamini kumwilisha upendo wa Mungu na kwa jirani zao na kwamba, vijana wa kizazi kipya ni mahujaji wa kwanza wa matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kongamano la Kitume: “Congrès Mission” lilianzishwa kunako mwaka 2015, huko Paris, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa njia ya ushirikiano wa vyama vya kitume na jumuiya mbalimbali za kimisionari nchini Ufaransa. Ni kongamano linalokita mizizi yake katika maisha na utume wa kimisionari, unaowataka Wakristo kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, tayari kumtangaza na kumshuhudia kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu. Kila mwamini anaweza kugundua mbinu ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, kwa kuzingatia utu wake na utume asilia. Mawasiliano huboreshwa zaidi na hivyo kuongeza shauku ya kimisionari, kwa kila mwamini kutambua kwamba anayo dhamana na wito wa kutekeleza katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, Kanisa linaheshimu na kuthamini mchango wa kila mwamini.

Furaha, matumaini na utume ni sawa na chanda na pete
Furaha, matumaini na utume ni sawa na chanda na pete

Ni katika muktadha wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, viongozi 50 wa Kongamano la Kitume kutoka Ufaransa, Ijumaa tarehe 10 Januari 2025 walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, kama sehemu ya maandalizi ya Kongamano la Kitume, litakaloadhimishwa kuanzia tarehe 7 hadi 9 Novemba 2025 huko Bercy Jijini Paris, Ufaransa kama sehemu muhimu sana ya kushirikishana uzoefu na mang’amuzi katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amewapongeza kwa uaminifu wao kwa Injili chemchemi na mwanga wa matumaini, Kristo Yesu ni tumaini la waja wake, lango la matumaini, chemchemi ya Habari Njema ya Wokovu. Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili mwaliko kwa waamini kumwilisha upendo kwa Mungu na kwa jirani zao na kwamba, vijana wa kizazi kipya ni mahujaji wa kwanza wa matumaini.

Upendo ni utambulisho wa Wakristo
Upendo ni utambulisho wa Wakristo

Baba Mtakatifu anasema maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa matumaini.” Matumaini haya yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu. Huu ni mwaliko kwa waamini kupyaisha maisha yao, kwa kujikita katika utume, ili hatimaye, waweze kuwa ni mahujaji wa matumaini yasiyodanganya kamwe. Furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu, wale wanaokubali zawadi yake ya ukombozi, wanawekwa huru. Rej Evangelii gaudium 1. Furaha, matumaini na utume ni mambo yanayokumbatiana na kukamilishana kwa kupata chanzo kutoka kwa Kristo Yesu na hivyo kujielekeza kwenda kwa jirani, ili kuwapelekea wengine matumaini ya Injili inayofariji na hatimaye, kufungua njia mpya. Utume ni uchu kwa ajili ya Kristo Yesu na uchu kwa ajili ya watu wake kwa wakati mmoja, kwa kusukumwa na upendo unaogeuka na kuwa ni utambulisho wao wa pamoja. Rej Evangelii gaudium, 268.

Kila mtu anapaswa kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa
Kila mtu anapaswa kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, fadhila ya matumaini inakabiliana na changamoto nyingi, mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni wajumbe wa matumaini nchini Ufaransa ambako kuna idadi kubwa ya watakatifu wa Mungu. Matumaini ni zawadi kutoka kwa Mungu inayopaswa kushirikishwa na mwanga unaopaswa kuongoza dira na mapito ya waamini. Roho Mtakatifu kama lilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo, ndiye mwalimu na mwinjilishaji mkuu anayewahamasisha waamini kutenda shughuli zao katika hali ya ubunifu mkubwa, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika upendo. Vijana wa kizazi kipya ndio mahujaji wa kwanza wa matumaini, wanayo kiu ya kutaka kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii. Baba Mtakatifu, anawahamasisha kujenga mahusiano na mafungamano yatakayowakutanisha na Kristo Yesu. Utume wa kimisionari uwawezeshe kujenga umoja na mshikamano; ushuhuda wa hali ya juu kabisa. Kristo Yesu anasema “Kama mkipendana ninyi kwa ninyi, kwa njia hii, watu wote watajua kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.” Yn 13: 35. Waamini wahakike kwamba wanajenga upendo kwa jirani zao katika furaha na magumu ya maisha, ili kuhakikisha kwamba matunda ya Roho Mtakatifu yanawafikia wengi. Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe, kufanya maandalizi ya kina kwa ajili ya maadhimisho ya Kongamano lao Mwenyezi Novemba 2025 na kwamba, atashiriki pamoja nao kiroho. Mwishoni mwa tafakari yake akawakabidhi wajumbe hawa kwa tunza na ulinzi wa Bikira Maria mwaminifu aliyebeba tumaini la Ulimwengu moyoni mwake na mikononi mwake, ili aweze kuambatana nao katika utume huu ndani ya Kanisa.

Kongamano la Kitume

 

 

14 January 2025, 15:00