ҽ

Harusi ya Kana ya Galilaya Ni Muhtasari wa Maisha na Utume wa Kristo Yesu

Baba Mtakatifu Francisko, katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika, tarehe 19 Januari 2025 amesema, ni katika harusi ya Kana ya Galilaya, Kristo Yesu alifanya ishara yake ya kwanza kwa kugeuza maji kuwa ni divai, akaudhihirisha utukufu wake na wanafunzi wake wakamwamini. Huu ni muhtasari wa maisha na utume wa Kristo Yesu, Ishara ya karamu ya uzima wa milele itakayoandaliwa na Mwenyezi Mungu. Hii ni karamu ya divai na vinono.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tafakari ya Injili ya Yohane 2: 1-11 Dominika ya Pili ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa inajikita katika ufunuo wa huruma, upendo na furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu anayefungua ukurasa mpya wa uwepo wa Mungu kati pamoja na waja wake. Huu ni mwaliko wa kuendelea kudumu katika uaminifu, upendo, umoja na mshikamano na Kristo Yesu chimbuko la ukombozi wa mwanadamu. Ishara ya Harusi ya Kana ya Galilaya ni kielelezo cha upendo na uaminifu wa Mungu kwa watu wake. Mwinjili Yohane anamweka mbele ya macho ya waamini Bikira Maria anayeguswa na mahitaji ya wanandoa wapya waliotindikiwa na divai na hivyo kuomba huruma na upendo wa Yesu kwa niaba yao! Divai ni ishara ya furaha na upendo, lakini wakati mwingine, mwanadamu anatindikiwa na divai, kumbe, katika muktadha huu, waamini wajifunze kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, atakayewaonesha uwepo wa Mungu katika safari ya maisha yao ishara ya: Imani, furaha, upendo na matumaini. Ujio wa Kristo Yesu ni chemchemi ya: Matumaini, upendo, furaha, huruma na utakaso katika maisha. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika, tarehe 19 Januari 2025 amesema, ni katika harusi ya Kana ya Galilaya, Kristo Yesu alifanya ishara yake ya kwanza kwa kugeuza maji kuwa ni divai, akaudhihirisha utukufu wake na wanafunzi wake wakamwamini. Huu ni muhtasari wa maisha na utume wa Kristo Yesu, Ishara ya karamu ya uzima wa milele itakayoandaliwa na Mwenyezi Mungu. Hii ni karamu ya divai na vinono. Rej Isa 25: 6. Kristo Yesu ndiye Bwana harusi wa Agano Jipya na la milele anayewaletea waja wake “divai iliyo njema” ya upendo wake wa daima, ili kupyaisha tena Agano la ndoa kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu.

Katika safari ya maisha kunakutindikiwa na divai!
Katika safari ya maisha kunakutindikiwa na divai!

Mwinjili Yohane anakazia kuwa ni “Ishara” na wala si muujiza unaonesha nguvu na ukuu wake, ili kuwashikisha watu tama kwa mshangao. Ishara hii ni mwanzo wa ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu unaodhihirisha ukaribu, upole na huruma ya Mungu kwa waja wake. Kristo Yesu anatenda ishara hii kwa wanandoa wapya, katikati kabisa ya furaha ya ndoa yao. Kutindikiwa divai, kungeharibu sherehe nzima na wageni waalikwa kuanza “kutupa vijembe.” Bikira Maria alikuwa wa kwanza kung’amua changamoto waliyokuwa wanakabiliana nayo wanandoa hawa wapya, akaamua kuingilia kati pasi na makuu wala kutaka “kujimwambafai” mbele ya wanandoa na wageni waalikwa, bali yote akayatenda katika hali ya kimya kikuu. Kristo Yesu akawaambia kuyajaliza mabalasi maji yaliyopata kuwa divai. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika sehemu hii ya Injili mambo makuu mawili yanajitokeza: “Kutindikiwa na Divai na wingi wa divai.” Baada ya kumsikiliza Mama yake, Kristo Yesu aliwaambia wajazilize mabalasi maji, yaliyogeuka kuwa ni divai nyingi kiasi cha kumshangaza mkuu wa meza na kuanza kumsifia Bwana harusi kwa kuweka divai iliyo njema hadi mwisho wa harusi, wingi wa divai ni alama ya uwepo wa Mungu, mwanzo wa karamu ya uzima wa milele. Pale mwanadamu anapotindikiwa, Mwenyezi Mungu anajaza neema na upendo wake. Rej Rum 5:20.

Ishara ya kwanza kutendwa na Yesu ni Muujiza wa Harusi ya Kana ya Galilaya
Ishara ya kwanza kutendwa na Yesu ni Muujiza wa Harusi ya Kana ya Galilaya

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata katika karamu ya maisha ya mwanadamu, kuna wakati anatindikiwa na divai, hasa pale hofu na mashaka yanapozidi, furaha na matumaini yanapoyeyuka na kutoweka kama “ndoto ya mchana.” Katika muktadha wa kutindikiwa huku, Mwenyezi Mungu anawajaza waja wake upendo kwa njia ya Roho Mtakatifu, chemchemi ya furaha na matumaini. Anawakirimia ili kamwe wasitindikiwe na karamu ya harusi iweze kusonga mbele. Waamini wanapaswa kujiuliza Je, ni wakati gani wametindikiwa furaha na upendo, wakawa tayari kumkimbilia Kristo Yesu? Je, wanapokirimiwa upendo, wanajitahidi kuuhifadhi katika sakafu ya maisha yao, tayari kuwashirikisha wale waliovunjika na kupondeka moyo, tone hilo la upendo? Katika hali ya mwanadamu kutindikiwa katika maisha, Mwenyezi Mungu anamkirimia Roho Mtakatifu, anayepyaisha maisha ya waja wake. Baba Mtakatifu amehitimisha tafakari yake, kwa kutoa mwaliko kwa waamini kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa divai mpya, ili aweze kuwaombea katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Bikira Maria awasaidie kugundua tena furaha ya kukutana na Kristo Yesu.

Harusi ya Kana
19 January 2025, 14:37

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >