Kuelekea ng’ambo ya II ya 2025
Na Padre Joseph Herman Luwela - Vatican.
Kisha kuanguka dhambini ahadi ya Baba ilikuwa Emanuel, Mungu pamoja nasi… Mfalme huyu mkuu yupo katika sura ya kitoto dhaifu… uchakavu wa ulimwengu na pendo lake Baba vimepelekea Mwana ashuke jinsi hiyo, afanane nasi katika yote (isipokuwa dhambi), abaki nasi, akitufundisha polepole maana ya ujio wake tupate kuongoka kutoka kutojiweza kwetu. Tunapotazama pango la Bethlehem tunaona Nuru halisi, ‘amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu… na wote wenye kumpokea wanapokea uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu’ (Yh 1:9, 12). Nuru hiyo ndiyo inayotuwezesha usiku huu kuvuka kuelekea ng’ambo ya pili, 2022... Nuru ya Kristo inatufanya tugeuze shingo zetu kuona yaliyojiri 2021 ili tujue mwendo wetu kwa sasa na kule tunakoelekea…
Mnamo mwaka 2021 ilikuwa bajaji iliyosheheni mengi, ya furaha na ya huzuni, mafarakano, mafanikio na kushindwa, heri na baraka, uonevu, ukwasi, umasikini, kukata tamaa, majeraha na msamaha, uasi na ukaidi.. pia imani na matendo mema… UVIKO-19 ilitulaza na viatu, kwa changamoto zake za upumuaji, kuambukizana, misiba ya ndugu, matumizi ya dawa na fedha, kulazwa na kuuguza muda mrefu, kujitenga, kusimama shughuli hasa makongamano, semina, michezo nk vilitufanya tujione, tujitathmini na kujijua tulivyo si chochote... ilituhusu wote, wakubwa na wenye vyeo, wadogo kadhalika… Ugonjwa huu umehubiri ukuu wa Mungu na mamlaka yake na kutukumbusha usikitu wetu, basi na tuuvae unyenyekevu na kuuishi utaua wa kimungu tukipendana kwa dhati yote... kwa tuliyofaulu utukufu na sifa ni kwake, kwa yaliyotuumiza ni ishara kwamba tunahitaji bado wongofu na msamaha.
Sisi tulio wazima wasaa huu tumeshikwa na mshangao unaoambatana na shukrani kwamba Mungu ametufikisha siku hii. Tunawakumbuka waliokwisha kuitwa kwake: wachungaji, viongozi wa siasa, watawa, makatekista, walimu, wahudumu wa afya, wafanyabiashara, wakuu na wenye vyeo, waseminari, wanafunzi, watoto wetu, wazazi, wenzi, ndugu na jamaa… katika hili tuseme na Mfalme Daudi “mimi ni nani Bwana Mungu, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hata hapa…” (2Sam 7:18, 1Nyak 17:16). “Mwaka mpya na mambo mapya!!” inawezekana? ni yepi hayo? kwa kila kitu! kwamba tutupilie mbali tulivyonavyo vyote na kununua vilivyo vipya? visufuria, vinguo, tuviatu na tukandambili, blanketi na shuka, mbwa, mbuzi na kuku, tubaiskeli na tupikipiki hata nyumba tunamojisitiri... halafu ndugu tulionao, hofu, mashaka, mahangaiko, mafarakano, kesi tulizonazo, mipango, vionjo na tabia... haya yote hata tufanye vipi yatabaki kuwa ya zamani, sio tu 2021 bali pengine zamani zaidi... Ni upya upi tunaouhitaji? ni upya wa roho, weupe wa moyo na wongofu wa kweli na wa ndani kwa vile “mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua yote” (Somo I - 1Yh 2:20).
Kuelekea ng’ambo ya pili, hatujui 2025 inatuletea nini, na hii huenda inatupa hofu... tusiogope, Bwana yu pamoja nasi... Katika Kristo ikawe safari njema, ikawe heri, safari ya imani na matumaini... Ikawe mwanzo mpya wa fikara na tafakari, wa tabia na maelekeo mema, wa fadhila na uchaji, wa hofu ya Mungu, wa ibada na matendo mema, mwanzo mpya wa kukua na kukomaa, kupiga hatua katika mema na udumifu katika kweli… Mungu Mkuu na atubariki katika nia yetu ya kuukubali maongozi na mapenzi yake katika mwaka mzima ujao, amina.
Heri sana kwa Mwaka Mpya 2025!