蜜桃交友

Tafuta

Makombora nchini Siria. Makombora nchini Siria.  (ANSA)

Syria:Makombora yashambulia vituo vya afya na kuacha madhara makubwa

Pamoja na vita vinavyoendelea huko Lebanon na Gaza,ni pia mapigano yanaendelea huko kaskazini-magharibi mwa Syria na ambayo yanaacha raia wameuawa,wengine wamejeruhiwa huku hospitali zikizidiwa uwezo kutokana na ongezeko la mashambulizi dhidi ya vituo vya afya.Umoja wa Mataifa unalaani vitendo hivyo.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akisema mara kadhaa kwamba "vita vya tatu vya dunia vimegawanyika vipande vipande," hii ni kweli kwamba kila wakati vinaibuka hapa na pale hata vilivyokuwa vimetulia kama volkano chini ya ardhi. Akitoa salamu mbali mbali kwa waamini waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, Papa Francisko kuhusiana na vita alisema "Na "tafadhali, tuendelee kuomba amani! Vita ni kushindwa kwa mwanadamu. Vita haisuluhishi shida, vita ni mbaya, vita huharibu. Tunaombee nchi zilizo kwenye vita. Tusisahau Ukraine inayoteswa, tusisahau Palestina, Israel, Myanmar... Watoto wengi waliokufa, wengi waliokufa wasio na hatia! Tuombe kwa Bwana atuletee amani. Daima tuombe amani,” Papa alikazia kusema. 

Vita nchini Siria

Ni katika muktadha huo wa vita ambapo kumeibuka tena huko Kaskazini-magharibi mwa Syria,  mapigano mapya yaliyoanza Juma lililopita yakiongozwa na kikundi cha kigaidi cha Hay’at Tahrir al-Sham (HTS) na vikundi vingine vilivyojihami ambavyo vimezingira maeneo ya miji ya Aleppo, Idlib na Hama, ambapo linakuwa tena jinamizi la mashambulizi kwenye maeneo ambayo yalikuwa kimya tangu mwaka 2020. Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, (OHCHR) Jeremy Laurence alieleza waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi tarehe 3 Desemba 2024 kwamba: “idadi kubwa ya matukio ya kutia hofu na kusababisha vifo vya  raia wengi, wakiwemo wanawake na watoto, inatokana na mashambulizi yanayofanywa na magaidi wa HTS na majeshi  yanayounga mkono serikali ya Syria. Uhasama unasababisha uharibifu wa miundombinu ya kiraia,  ikiwemo vituo vya afya, majengo yenye taasisi za elimu, na masoko ya chakula,” alisisitiza kiongozi huyo. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu(OHCHR) tayari imeanza mchakato wa kuthibitisha mashambulizi makubwa yanayodhuru raia, ikiwemo vifo vya raia wanaume wanne tarehe 29 Novemba 2024,  na “vinavyodaiwa kutokea kufuatia makombora kadhaa yaliyorushwa ardhini na HTS,” na kupiga eneo lenye mabweni ya Chuo Kikuu cha Aleppo”, alisema  msemaji huyo wa OHCHR.

Makombora kuharibu chuo Kikuu cha Aleppo

Katika taarifa zilizokusanywa na ofisi hiyo zinasema kuwa watu wote hao wanne waliikuwa wanafunzi wa Chuo hicho Kikuu, na kufuatia tukio hilo, wanafunzi wengi wamekimbia eneo hilo la chuo. Kwa upande wa Jens Laerke, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, (OCHA), alisisitiza kuwa hali katikaeneo hilo bado ni tete na inabadilika mara kwa mara. Wakati OCHA ina mtandao thabiti ndani ya Syria na kwenye maeneo ya mpakani na kituo cha misaada ya kibinadamu cha Gaziantep, nchini Uturuki, imelazimika kusitisha operesheni zake, “kwa sababu ya ukosefu wa usalama,” kutokana na mapigano yanayoendelea na barabara nyingi zimefungwa. Hata hivyo alisema, “si eneo lote ambalo limekumbwa na vizuizi. Bado kuna maeneo ambako unaweza kupeleka misaada, kwa mfano katika  vituo vya mapokezi vya Idlib ambako kuna watu waliokimbia makazi yao kutokana na ghasia.”

Kwa mujibu wa OCHA, watu wa Syria  wapatao milioni 16.7 tayari wanahitaji msaada wa kibinadamu tangu kuanza mwaka huu wa 2024. Msemaji wa OHCHR, Bwana  Jeremy Laurence pia aliakisi tukio la  tarehe 1 Desemba 2024, ambapo raia 22 waliuawa, wakiwemo wanawake watatu na watoto saba, na raia wengine 40 walijeruhiwa, “ikiripotiwa kuwa ni kutokana na makombora kadhaa yaliyorushwa kutoka angani na vikosi vinavyounga mkono serikali ya Syria. Makombora hayo yaliangukia mji wa Idlib, kwenye eneo lenye soko na makazi ya watu. Tunakumbusha pande husika juu ya wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu na sheria za kibinadamu: raia na miundombinu ya kiraia lazima ilindwe,” alisisitiza.

'Ukatili wa miaka ya nyuma haupaswi kurudi tena Syria'

Akipazia sauti wito huo, Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Kuchunguza Syria imeonya kupitia taarifa yake ya tarehe 3 Desemba 2024 kuwa: “ukatili wa miaka ya nyuma haupaswi kurudiwa, au Syria itatumbukizwa kwenye mweneleo mpya wa mauaji.” Zaidi ya vituo vya afya 100 kwenye mji wa Aleppo, ambao makazi ya watu zaidi ya milioni 2, “hospitali zinazofanya kazi ni chini ya 8 na zinatoa huduma chini ya kiwango,” alisisitiza Bi  Christina Bethke, Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO, nchini Syria. Mathalani shambulio la Jumatatu huko Idlib limeharibu miundombinu ya afya kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu, Hospitali ya Wazazi na ofisi ya utawala na usimamizi wa afya kwenye eneo hilo. Tangu tarehe 27 mwezi uliopita wa Novemba, WHO imepokea ripoti za mashambulio yapatayo sita dihdi ya vituo vya afya Syria. Bi. Bethke amesisitiza kuwa vituo vya afya vinalindwa kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu.

04 December 2024, 17:57