蜜桃交友

Tafuta

Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amemteua Balozi Mahmoud Thabit Kombo kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amemteua Balozi Mahmoud Thabit Kombo kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  

Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amemteua Balozi Mahmoud Thabit Kombo kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akichukua nafasi ya January Yusuf Makamba ambaye uteuzi wake umetenguliwa. Kabla ya uteuzi huu Balozi Kombo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia. Katika kipindi chake cha uongozi kama Balozi ameonesha jitihada za ujenzi wa umoja na mshikamano wa watanzania diaspora.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amemteua Balozi Mahmoud Thabit Kombo kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akichukua nafasi ya January Yusuf Makamba ambaye uteuzi wake umetenguliwa. Kabla ya uteuzi huu Balozi Kombo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia. Hivi karibuni Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia, aliwataka watanzania kuchangamkia fursa za masomo zinazotolewa na Taasisi mbalimbali nchini Italia, ili kuwaandaa viongozi watakaojisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania. Anatambua kwamba, kama Mapadre wanayo dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Lakini uongozi wa maisha ya kiroho una mchango mkubwa katika kukoleza: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika masuala ya uchumi, haki, amani na utulivu wa nchi. Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Kanisa Katoliki katika maendeleo ya watanzania katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Ili kuweza kufikia hapa kuna haja ya kupambana na “ukweli mchungu” unaokita mizizi yake katika uchoyo na uroho, mambo yanayosababisha athari za mabadiliko ya tabianchi na watu kushindwa kuwashirikisha wengine kuchangia fursa za masomo nchini Italia.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alipotembelea Vatican 18.02.2024
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alipotembelea Vatican 18.02.2024

Tangu mwanzo wa mchakato wa uinjilishaji nchini Tanzania, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hususan katika nyanja za elimu, afya, maendeleo na ustawi wa jamii, bila kusahau huduma ya maisha ya kiroho kwa watu wa Mungu nchini Tanzania na katika mchakato wa kudumisha amani ulimwenguni. Takwimu zinaonesha kwamba, Kanisa Katoliki nchini Tanzania hadi kufikia mwaka 2024 linamiliki na kuendesha shule za awali 240, shule za msingi 147, shule za sekondari 244, vyuo vya ufundi, vyuo vikuu 5; taasisi za elimu ya juu 5 na vituo vya vyuo vikuu 2 ambavyo viko chini ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, SAUT. Vyuo vyote hivi vina jumla ya wanafunzi 31, 000 pamoja na taasisi za afya ni 473, lengo likiwa ni kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi, utenguzi na uhamisho wa viongozi mbalimbali. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Dominika tarehe 21 Julai 2024 viongozi hao ni kama ifuatavyo:

(i) Mhe. Jerry William Silaa (Mb.) ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Kabla ya uteuzi huu Mhe. Silaa alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, anachukua nafasi ya Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb.) ambaye uteuzi wake umetenguliwa;

(ii) Mhe. Deogratius John Ndejembi (Mb.) ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kabla ya uteuzi huu Mhe. Ndejembi alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu);

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alipokutana na Baba Mtakatifu Francisko
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alipokutana na Baba Mtakatifu Francisko

(iii) Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mb.) ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu). Kabla ya uteuzi huu Mhe. Kikwete alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora;

(iv) Mhe. Cosato David Chumi (Mb.) ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Mhe. Chumi anachukua nafasi ya Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ambaye atapangiwa kituo cha kazi;

(v) Mhe. Deus Clement Sangu (Mb.) ameteuliwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora;

(vi) Mhe. Dennis Lazaro Londo (Mb.) ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki. Mhe. Londo anachukua nafasi ya Mhe. Stephen Lujwahuka Byabato (Mb.) ambaye uteuzi wake umetenguliwa;

(vii)Bw. Eliakim Chacha Maswi ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria. Kabla ya uteuzi huu Bw. Maswi alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA);

Waziri mkuu alipotembelea Kanisa kuu la Mt. Petro
Waziri mkuu alipotembelea Kanisa kuu la Mt. Petro

(viii) Bi. Mary Gaspar Makondo ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma. Kabla ya uteuzi huu Bi. Makondo alikuwa Katibu Mkuu wa

Wizara ya Katiba na Sheria. Bi. Makondo anachukua nafasi ya Bi. Rehema Sefu Madenge ambaye amestaafu;

(ix) Bw. Kiseo Yusuph Nzowa ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro. Kabla ya uteuzi huu Bw. Nzowa alikuwa Afisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais – Ikulu;

(x) Bw. Musa Haji Ali ameteuliwa kuwa Balozi. Kabla ya uteuzi huu Bw. Ali alikuwa Afisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais – Ikulu;

(xi) Bw. Louis Peter Bura ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato. Bw. Bura anachukua nafasi ya Bw. Said Juma Nkumba ambaye amepangiwa majukumu mengine;

Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia 25 Mei 2024
Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia 25 Mei 2024

(xii) Bi. Kemirembe Rose Lwota amehamishwa kutoka Wilaya ya Manyoni kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti;

(xiii) Dkt. Vincent Biyegela Mashinji amehamishwa kutoka Wilaya ya Serengeti kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya Manyoni;

(xiv) Dkt. Maulid Suleiman Madeni ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti;

(xv) Bw. Afraha Nassoro Hassan amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi. Bw. Hassan anachukua nafasi ya Bw. William Anyitike Mwakalambile ambaye uteuzi wake umetenguliwa; na

(xvi) Bw. Dennis Kwame Simba ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA). Kabla ya uteuzi huu Bw. Simba alikuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).

Tanzania
22 July 2024, 16:36