Uwekezaji Katika Silaha ni Hatari Kwa Ustawi, Mafao na Maendeleo ya Wengi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Cattolica Assicurazioni yaani “Bima ya Kikatoliki” ilianzishwa kunako mwaka 2006 kama kielelezo cha wajibu wa kijamii wa Bima ya Kikatoliki ambayo sasa ni kitengo cha biashara cha Kampuni ya “Generali Italia S.p.A,” ili: kujibu mahitaji ya ndani, kutunza watu na kuchangia kuweka hisia za jamii hai ndani ya Jumuiya za waamini wa Kanisa Katoliki. Huu ni utume unaojengwa juu ya kanuni maadili, ili kukuza na kudumisha maendeleo jamii kwa kiwango cha kibinadamu, utu, heshima, hadhi na wito wake wa kuwekeza katika kazi zinazoakisi maadili mema, mshikamano, ushirikiano, uhuru na udugu wa kibinadamu. Yote haya yamejengeka juu ya majibu ya mahitaji ya ndani, kwa kuwajali watu na hivyo kuchangia kuwekeza hisia za jamii hai.
Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa matumaini.” Matumaini ya waamini yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu aliyezaliwa katika Familia Takatifu iliyopata baraka ya kuwa na Mungu yaani Emanueli kati yake. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo wajumbe wa “Cattolica Assicurazioni” yaani “Bima ya Kikatoliki,” Jumamosi tarehe 18 Januari 2025 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.
Katika hotuba yake amekazia umuhimu wa jamii kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote, kama sehemu muhimu sana ya kukuza uchumi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uwekezaji katika utengenezaji wa silaha ni hatari kwa ustawi, mafao na maendeleo ya binadamu na kwamba, wanao wajibu wa kuwekeza amana na utajiri wao katika utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha wajumbe wa Bima ya Kikatoliki kwamba, wamepewa dhamana ya kulinda na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote, nyumba ambayo pia ni ya kijamii. Bima ya Kikatoliki inaendelea kujikita katika ujenzi wa mshikamano, kwa majitoleo ya wtu, malezi na majiundo ya kitamaduni na kitaalam, lakini zaidi, kwa kuendelea kuunga mkono ustawi na maendeleo ya familia na vijana wa kizazi kipya, kwa kushirikiana kwa karibu sana na Jimbo Katoliki la Verona.
Huu ni ukaribu wa Kikatoliki, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, hiki ni kielelezo makini cha programu ya maisha. Baba Mtakatifu anawataka wajumbe hawa kuwekeza zaidi katika uaminifu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani zao. Inasikitisha kuona kwamba, kuna nchi nyingi duniani ambazo zinaendelea kuwekeza katika utengenezaji wa silaha duniani zenye lengo la kusababisha mauaji na kwamba, waathirika wakuu ni maskini, “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.” Waathirika wakuu wa tabia ya uchoyo na ubinafsi ni maskini. Kumbe, hii ni changamoto kwa wawekezaji kuwekeza amana na utajiri wao kwa ajili ya huduma kwa utu, heshima, ustawi na maendeleo ya binadamu. Na kwa njia hii, waweza kujikita katika kutafuta na kudumisha mafao ya wengi, tayari kushiriki katika maboresho ya maisha ya watu, ili kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika upendo na haki. Baba Mtakatifu amewapongeza kwa kuendelea kuwekeza katika furaha, amani ustawi na maendeleo ya jirani zao.