Papa Francisko:Na tusiache kuombea amani na tusisahau kuwa vita siku zote ni kushindwa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika siku ambayo Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, tarehe 12 Januari 2025, Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana alianza kusema: “Niko karibu na wakazi wa Kaunti ya Los Angeles, California, ambako hivi karibuni moto mkali umepamba moto” na hivyo "Tuwaombee."
Ubatizo wa watoto
Papa aliendelea kusema kuwa: “Asubuhi ya leo nilikuwa na furaha ya kuwabatiza baadhi ya watoto wachanga, watoto wa wafanyakazi wa Vatican na wa Walinzi wa Uswisi. Tunawaombea wao, na familia zao. Na ningependa kumwomba Bwana, kwa wanandoa wote vijana wapate furaha ya kukaribisha zawadi ya watoto na kuwaleta kwenye Ubatizo."
Mwenyeheri mpya Yohane Merlini
Katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane Laterano, Papa lisema " asubuhi ya leo Padre Giovanni Merlini, Padre wa Wamisionari wa Damu Azizi, alitangazwa kuwa Mwenyeheri. Akiwa amejitolea kwa ajili ya utume kwa watu, alikuwa mshauri mwenye busara kwa nafsi nyingi na mjumbe wa amani. Pia tunaomba maombezi yake tunapoombea amani nchini Ukraine, Mashariki ya Kati na duniani kote. Mzunguko wa makofi kwa Mwenyeheri mpya!”
Salamu kwa mahujaji
Papa amewasalimu wote kuanzia na Warumi na mahujaji, hasa wanafunzi wa Olivenza, Hispania, na wana Familia ya Wafuasi pamoja na walei wanaofanya kazi katika nyumba za Kazi ya Padre Semeria na Padre Minozi. Papa alisisitiza kuwa: “Na tusiache kuombea amani na tusisahau kuwa vita siku zote ni kushindwa. Ninawatakia wote Dominika njema. Na tafadhali msisahau kuniombea. Mlo mwema, mchana mwema na kwaheri ya kuonana."