蜜桃交友

Tafuta

2022.11.25 Dominika ya Kwanza ya Majilio 2022.11.25 Dominika ya Kwanza ya Majilio 

Majilio:Kipindi cha kuamka Kiroho na kujiandaa kwa ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo

Majilio ni kipindi cha matumaini,mapendo,imani,toba na maandalizi ya ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo;ni kipindi cha kutafakari na kujiandaa kwa matukio mawili makubwa ya imani yetu.Kuishi Majilio ni kutembea kuelekea Noeli kwa moyo wazi na tayari kupokea neema ya Kristo

Na Padre Philemon Antony Chacha-Shirika la Wasalesian wa Don Bosco

Mwenyezi Mungu, katika ukarimu Wake usio na kipimo, ametuzawadia na anazidi kutuzawadia muda mwingi zaidi ili tuweze kumjua na kumpenda yeye kwa undani. Dominika tarehe 1 Desemba 2024, Jumapili ya Kwanza ya Majilio, tunaanza mwaka mpya wa Kanisa na wa kiliturujia ambao ni mwaliko wa kina kwetu sote, kuzama katika fumbo la Kristo, tukijifunza kutoka katika Neno Lake na kushiriki katika Sakramenti. Mama Kanisa, anatupatia mwongozo katika safari hii ya kumkaribia Mungu katika kipindi cha Majilio. Hivyo ni wakati wa kutafakari na kujiandaa kwa ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo, huku tukimruhusu Yeye azaliwe tena upya katika maisha yetu. Pia ni wakati wa kusafisha mioyo yetu kwa toba na kuhuisha maisha yetu kwa kutafakari na kushuhudia ujio mbalimbali wa Kristo katika maisha yetu.

Je neno Majilio lina maana gani? Majilio ni neno linatokana na neno la Kilatini “adventus” lenye maana ya “kuja” au “kuwasili”. Katika lugha ya Ulimwengu wa Kale lilikuwa neno la kitaalamu lililotumika kuonesha kuwasili kwa ofisa au ziara ya mfalme katika jimbo. Wakristo walichukua neno “ujio” ili kueleza uhusiano wao na Yesu Kristo: Yesu ndiye Mfalme, ambaye aliingia katika “jimbo” maskini linaloitwa dunia, ili kumtembelea kila mtu, na kuwaalika wamwaminio kushiriki katika Sherehe ya ujio wake. Kumbe, Majilio ni kipindi cha matumaini, mapendo, imani, toba na maandalizi ya ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo; ni kipindi cha kutafakari na kujiandaa kwa matukio mawili makubwa ya imani yetu. Kwanza, tunajiandaa kusherehekea ujio wa Kristo kwa mara ya kwanza katika sikukuu ya Noeli, ambapo Mwenyezi Mungu alikubali kuja duniani kama mwanadamu. Pili, Majilio hutuongoza kuelekea katika ujio wa Kristo kwa mara ya pili, wakati wa utukufu, mwishoni mwa nyakati, “kuwahukumu wazima na wafu” kama tunavyosali kila Jumapili katika sala ya kukiri Imani.

Kipindi cha Majilio kina tabia za aina mbili, kwanza ni Kipindi cha maandalizi kwa ajili ya Sherehe ya Kuzaliwa kwa Bwana, ambapo Ujio wa Kwanza wa Mwana wa Mungu kwa binadamu unakumbukwa, na vivyo hivyo ni Kipindi ambacho, kwa kulikumbuka fumbo hili, akili na mioyo yetu inaongozwa kuungojea ujio wa Kristo kwa mara ya pili yaani mwisho wa nyakati. Kwa sababu hizi mbili, Majilio ni kipindi cha uchaji na kungojea kwa furaha kuu. Majilio yanaanza na Vesperi ya Kwanza ya Dominika inayoangukia karibu na 30 Novemba na Kipindi hiki kinafungwa kabla ya Vesperi ya kwanza ya Kuzaliwa kwa Bwana. Siku za Juma zilizomo katika Kipindi cha kuanzia tarehe 17 Desemba hadi, na ikiwemo tarehe 24 Desemba zimepangwa moja kwa moja kwa maandalizi ya Kuzaliwa kwa Bwana.

Kipindi hiki kwanza kinatupatia fursa ya kutafakari vipaumbele vyetu, kujitakasa kwa kumfungulia nafasi Bwana anayekuja. Huu ndio mchakato wa kugeuza moyo—kuacha yale yasiyo ya muhimu na mabaya, ili tuweze kupokea Neema ya Mungu. Pili, Majilio yanatualika kuwa na uvumilivu. Mtume Paulo anatusihi tusikubali majaribu ya kuacha safari yetu ya imani, hata pale tunapokumbana na changamoto. Uvumilivu ndio unaotuwezesha kubaki waaminifu kwa Kristo hata wakati wa matatizo na changamoto mbalimbali za maisha. Katika Injili ya Luka (21:34-36), Yesu anatuonya tusiruhusu mioyo yetu kuwa mizito kwa anasa za dunia, bali tuwe macho na tuombe ili kupata nguvu za kukabiliana na majaribu. Hivyo, Majilio ni wakati wa kukuza bidii na uvumilivu. Bidii ya kila siku inatuandaa kwa ajili ya kuja kwa Bwana, wakati uvumilivu unatusaidia kudumu katika safari ya imani. Kuishi Majilio ni kutembea kuelekea Noeli kwa moyo wazi na tayari kupokea neema ya Kristo. Ni wakati wa matumaini na mabadiliko, si kusubiri bure bali kusubiri kwa matumaini.

Na mwisho, kipindi cha Majilio kinatuhimiza kutafakari kwa undani mwelekeo wa maisha yetu. Maisha yetu yana lengo. Hivyo, Noeli inatukumbusha kwamba Mungu alikuja duniani kutuokoa na kutuongoza kwenye uzima wa milele. Majilio yanatufundisha kuishi kwa uhakika huu, tukitembea kwa bidii na uvumilivu, tukijua kwamba Bwana hatachelewa kuja.

Baba Mtakatifu Francisco anatuambia kuwa: “Katika kipindi hiki cha Majilio tuamke kutoka usingizini! Tujiulize: Je, ninafahamu kile ninacho kiishi, je, nipo makini, je, nipo macho? Je, ninajaribu kutambua uwepo wa Mungu katika hali yangu ya maisha ya kila siku, au ninaangamia na kujichanganya na mambo ya ulimwengu? Ikiwa hatutambui ujio wake leo, tutakuwa hatujafanya maandalizi ya kutosha hata wakati atakapokuja kwa mara ya mwisho. Kwa hiyo, ndugu zangu, tuwe macho! Tukisubiri Bwana aje, tukisubiri Bwana akaribie na kukaa pamoja nasi...” (Sala ya Malaika wa Bwana, tarehe 27 Novemba 2022). Hivyo tuombe neema ya Mungu ili kipindi hiki cha Majilio kiwe kipindi cha kuamka kiroho, na tujiandae kwa ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa mioyo iliyo tayari kupokea neema zake.

Tafakari ya majilio na Padre Chacha

 

01 December 2024, 15:48