蜜桃交友

Tafuta

Tafakari ya Dominika ya 32 ya Mwaka B wa Kawaida:Injili ya mwanamke mjane,alitoa kila kitu alichokuwa nacho. Tafakari ya Dominika ya 32 ya Mwaka B wa Kawaida:Injili ya mwanamke mjane,alitoa kila kitu alichokuwa nacho. 

Huyu mjane masikini ametia zaidi kuliko wote

Biblia inataja wageni,yatima na wajane kama wanyonge wa jamii(Kumb 14:29).Na pia wote wanaosikumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na uduni wa hali zao.Wajane wa Salepta na wa Injili wanawakilisha makundi yote ya wanyonge wa jamii,tukae nao vizuri,tuwapende na tuwashike mkono sababu Mungu ndiye Mwamuzi wao,sala zao nyonge zinafika haraka mbele ya kiti cha enzi naye anawasikiliza mapema.

Na Padre Joseph Herman Luwela - Vatican.

Karibu tena mpendwa msikilizaji na msomaji wa tafakari ZETU, kutoka Radio Vaticano. Leo Kristo ana jambo lake leo kuhusu, majitoleo yaani sadaka kamili, kwamba tusiwe wanafiki tunaovaa mavazi marefu kama mafarisayo na kusalimiwa sokoni, kuketi mbele kwenye sinagogi na sherehe na kusali sala ndefu kwa unafiki, hukumu ni kubwa. Kwa mavazi hayo ni ngumu kufanya kazi, hivi uvivu ni dhahiri. Ili kupata heshima tutatamani mialiko, ugeni rasmi na vinono vya meza kuu… muhimu ni utumishi na majitoleo ya kweli, huduma bora na matendo ya haki na adili. Biblia inataja wageni, yatima na wajane kama wanyonge wa jamii (Kumb 14:29)…na pia wote wanaosikumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na uduni wa hali zao. Msisitizo wa Kristo leo ni juu ya  “… huyu mjane masikini ametia zaidi kuliko wote” (Mk 12:43)

UFAFANUZI

Mjane wa Salepta katika somo I (1Fal 17:10-16) na wa Injili (Mk 12:38-44) ni mfano halisi wa sadaka na majitoleo. Mjane wa Salepta alimpa Nabii wa Mungu Eliya chakula chake cha mwisho akabarikiwa kwa kutoishiwa unga na mafuta hadi mvua iliponyesha. Unga na mafuta ni chemchemi ya sakramenti inayobubujika bila kikomo, pasi kukauka kwa wote wanaoamini... Mjane wa Injili aliyetoa senti 2 ni Kanisa linalojitoa lenyewe kwa Mungu na kuwapa waamini vyote lilivyo navyo yaani huduma kupitia sakramenti, ibada, baraka, ushauri, maamuzi, changamoto za waamini na huduma za jamii (elimu, afya, maji nk) bila ubaguzi. Senti 2 za mjane ni maagano 2 ya Biblia, la Kale na Jipya... senti moja inawakilisha imani na nyingine neema. Yesu anamsifu kuwa ametoa kuliko wote kwa vile katika umasikini wake ametoa yote bila kubakiza kitu, sawa na kutoa maisha yake, asijue nini kitafuata baada ya hapo, alitoa kwa moyo wote na kwa nia njema tofauti na waliotoa nyingi lakini ziada.

Hakujua amesifiwa na Kristo hadi alipofika mbinguni na kupokea mara 100. Paroko, wako au padri mwadhimishi, au yeyote hajui umetoa kiasi gani na kwa nia ipi ila Kristo anajua. Kumbe Kristo anaangalia utoaji wetu, anakagua nia yetu ya utoaji, anajua tunatoa kwa moyo, kwa kujionesha, tunamtolea tulivyo navyo au ziada inayotubakia, tunatoa kwa uaminifu au kwa machungu, makasiriko, uzito na lawama... kama mjane yule sisi pia hatujui jinsi Kristo anavyotusifu mbele ya malaika na watakatifu kila wakati tunapotenda mema na tunaongezewa mara dufu kwani ukarimu na wema kwa jirani na kanisa hata jamii kwa ujumla havijawahi kuwa sababu ya umasikini kwa yeyote badala yake huwa baraka na Neema juu ya neema (2Kor 9:7) 

Katika maisha tuone umuhimu wa kulitegemeza Kanisa kwa zaka, sadaka na huduma… Kuna wimbo unaimbwa “usibanie za kunywea...” na mwingine “utakapokufa leo mali hiyo itakuwa ya nani?” … moyo na nia njema ya kusaidia kama wa wajane wa Salepta na wa Injili masikini ndio unaohitajika na ndio anaoupongeza Yesu. Kwa neno hili tuguswe moyoni na kumtolea Mungu kwa ukarimu wote. Wajane wa Salepta na wa Injili ni shule ya majitoleo, kati ya senti 2 angeweza kubakiza 1 lakini alitoa zote… anatufundisha kuwa watu tunaojitoa bila kujibakiza katika mambo mema na mazuri. Je, maisha yako yamepambwa na kunurulishwa na sadaka yoyote? Ni yapi majitoleo yako kwa Mungu, Kanisa na jirani? Ni watu wa aina gani unaowasaidia? Ni wenye uwezo wa kukulipa au hata masikini wasioweza kukupa kitu kwa vile hawana kutokana na hali zao? Maisha yetu ni sadaka, na tujitoe kwelikweli.

Mjane wa Injili anashangaza jambo moja, kutoa yote bila kubakiza chochote. Hivi tumejitoa kweli kwa Kristo? Ni jambo lipi tumebakiza na hatutaki kumkabidhi? umempa Yesu moyo wako na roho yako yote? Unazo senti 2, mpe Yesu zote na sio moja na wewe ubaki na moja yaani usiwe Mkristo nusu nusu. Sadaka yoyote inadai majitoleo… ukipata shida yoyote mf. huzuni, majonzi, hali ngumu, matatizo, mawazo, sintofahamu nk usilie kwa maumivu kama wanavyoumia wanyama wasio na utashi. Ili mateso yako yawe na faida uyatoe sadaka kwa Mungu kwa nia fulani, wengine husema “maua kwa Bikira Maria” mf. malipizi, wongofu wa wasioamini/wakosefu, marehemu toharani, amani, kwa ajili ya Kanisa na ustawi wake dhidi ya mashambulio kutoka ndani na nje, uadilifu wa viongozi wa dini/serikali. Usiteseke bure, tolea mateso hayo kama sadaka kwa Mungu wako.

Sadaka na majitoleo visambae baina ya wanandoa. Mmoja alisema mwenzi wako akigundua unampenda atakudharau na kukusumbua hivi upendo wake 50-50, mguu nje mguu ndani, hakuna tena zawadi, chocolato wala maua ukulinganisha wakti wa uchumba na urafiki zile ahadi na kumakinika kwa mwingine haipo sasa ni vitimbi na mikasa lawama chungu nzima kila mmoja naanza kujiuliza hivi ni huyu kweli? Ndi huyo na hiyo ndio rangi yake na ulisema ndio chaguo lake komaa nae sasa mkabidhi kwa Kristo mbadilisha vitu vyote na kuwa na imani na matumaini yasiyotayaharika. Wajane wa Salepta na wa Injili wanawakilisha makundi yote ya wanyonge wa jamii, tukae nao vizuri, tuwapende na tuwashike mkono sababu Mungu ndiye Mwamuzi wao, sala zao nyonge zinafika haraka mbele ya kiti cha enzi naye anawasikiliza mapema (Zab 146:9).

Mungu mwema atujalie roho ya kujisadaka, kuwaka ili kuangaza, sasa na siku.

Tafakari ya Neno la Mungu ya Dominika ya 32 Mwaka B wa Kanisa
08 November 2024, 14:26