蜜桃交友

Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 30 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo! Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 30 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo!  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tafakari Dominika 30 ya Mwaka B wa Kanisa: Injili ya Matumaini

Mama Kanisa katika Injili ya Marko 10: 46-52 anatuwekea mbele ya macho yetu, Kipofu Bartimayo Mwana wa Timayo kama kielelezo cha imani na matumaini kwa Kristo Yesu Mwana wa Mungu aliye hai. Kristo Yesu alikuwa anasafiri kutoka Yerusalemu pamoja na wanafunzi wake na mkutano mkubwa, huku akielekea kukabiliana na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu! Kanisa linahitimisha maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu! Mwanzo mpya!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Mpendwa sikilizaji na msomaji Radio Vatican, Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yamenogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Watu wa Mungu wakajitambua kuwa wao ni sehemu ya Kanisa la Kimisionari na Kisinodi, tayari kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu, kwa kushirikiana na binadamu wote, kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini kile ambacho Roho Mtakatifu anataka kuyaambia Makanisa. Huu ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliyozinduliwa kunako mwaka 2021 na unafikia kilele chake Dominika tarehe 27 Oktoba 2024 kwa Ibada ya Misa Takatifu inayotarajia kuanza saa 4:00 za Asubuhi kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 5:00 kwa Saa za Afrika Mashariki. Mama Kanisa katika Injili ya Marko 10: 46-52 anatuwekea mbele ya macho yetu, Kipofu Bartimayo Mwana wa Timayo kama kielelezo cha imani na matumaini kwa Kristo Yesu Mwana wa Mungu aliye hai. Kristo Yesu alikuwa anasafiri kutoka Yerusalemu pamoja na wanafunzi wake na mkutano mkubwa, huku akielekea kukabiliana na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu! Bartimayo Mwana wa Timayo aliposikia kwamba, Yesu anapita, akapiga kelele “Mwana wa Daudi Yesu, Unirehemu.” Wakataka kumnyamazisha, lakini yeye akapaaza sauti na kuvunjilia mbali viunzi na vizingiti vilivyokuwa vinamzuia, kiasi kwamba, Kristo Yesu, akaisikia na kujibu sauti yake. Hii inaonesha kwamba, Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima; ni mwanga wa mataifa na kiini cha Habari Njema ya Wokovu.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu: Umoja, Ushiriki na Utume
Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu: Umoja, Ushiriki na Utume

Tunakumbushwa kwamba, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, daima anasikiliza kilio cha maskini, wanapomlilia kwa imani na matumaini kama alivyofanya Kipofu Bartimayo Mwana wa Timayo, ambaye hakuogopa kupaaza sauti na hatimaye, kusikilizwa na Kristo Yesu kwa imani thabiti, kiasi cha kubisha hodi katika moyo wa Mwenyezi Mungu, licha ya kutoeleweka na mapingamizi aliyokutana nayo njiani. “Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona. Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani.” Mk 10: 51-52.Watu wanamkataza yeye anaita tu… nawe mkristo unayenisikiliza au kusoma tafakari hii usikubali “watu” wakuzuie au kukukatisha tamaa katika ndoto zako za kumkaribia Yesu na kujieleza hitaji lako kwa Imani na uhuru kamili : sali, kazana, vumilia, fanya hima… Kisha Kristo anamwita, watu wanageuka tena na kumwambia “Jipe moyo, inuka anakuita”... Tujifunze kuwapa moyo wenzetu, tusiwavunje moyo, siku yako isipite bila kumfariji yoyote alye karibu yako wengi wanaotuzunguka wanashida mbalimbali wanahitaji neno la Faraja na kutiwa moyo hata kama tunatofauti kwani upendo huvulia yote, huwezi jua unaweka uzima kiasi gani unapomwambia mtu aliyekata tamaa “Jipe moyo, inuka anakuita” ni faraja na matumaini kama tunavyonogeshewa na kauli mbiu ya mwaka wa Jubilee ya 2025 ya Ukristo isemayo “Matumaini hayatayahariki” ni sawa tu na alivyo ambiwa Bathimayo Jipe Moyo inuka anakuita.”

Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo!
Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo!

UFAFANUZI: Kisha kuponywa mwana huyu wa Timayo hageuki kushoto wala kulia, haendi nyumbani, anamfuata Yesu. Kumfuata Kristo ni ishara ya maisha mapya, upya wa roho, usafi wa moyo, nuru ya akili na afya ya mwili. Licha ya kuwa kipofu Bartimayo anamtambua Kristo vizuri na kwa uhakika kuliko wenye macho. Je, tunatambua kweli, kuhisi na kuonja uwepo wa Kristo kati yetu na zaidi sana katika Sakramenti Kuu ya Altare? tujizamishe ndani yake tupokee uponyaji wa roho zetu.  Anapoitwa anatupa joho lake. Joho lilikuwa vazi mchana na godoro usiku lililolaliwa nusu na nusu nyingine kujifunika. Likiwekwa rehani lilipaswa kurudishwa jioni ili mdaiwa asilale sakafuni kama tuonavyo katika somo 1 (Kumb 24:12-13). Anapoitwa na Yesu halikunji vizuri na kumpa mtu wa karibu akisema “naomba unishikie nakuja sasa hivi” analitupa na kumkimbilia Yesu. Tendo hilo lina maana ya kuachana na utambulisho wake kama ombaomba, kuachana na mali yake amfuate Yesu. Hili ni simulizi la ubatizo wa mtu anayeuvua utu wa zamani na kuuvaa utu mpya. Je, sisi leo tunaitikiaje wito wa Mungu wa kuachana na maisha ya zamani ili kuishi maisha mapya? tunapoambiwa “Jipe moyo inuka anakuita” tunakuwa wepesi na kutupa majoho yetu (mizigo, dhambi/tabia Fulani, uonevu kwa wengine hasa wanyonge walio chini yetu, uvunjifu wa haki, rushwa, uchochezi na yote yanayofanana na hayo) au tunataka tuyakunje kwanza ndipo twende kwa Yesu?

Injili ya matumaini inapaswa kutangazwa na kushuhudiwa
Injili ya matumaini inapaswa kutangazwa na kushuhudiwa

Mara nyingi tunajisikia hamu ya kuokoka, kuachana na tabia na mazoea Fulani mabaya na mazingira ya dhambi lakini bado tumekuwa wazito kuitikia tunasema “subiri kwanza, nina jambo langu nalimalizia” hadi fursa inapotea na pengine isirudi tena. Bartimayo aliwaza “nafasi ndio hii tu, haiji mara mbili, hakuna cha kunizuia” akapata kuona. Muujiza wa leo unatufundisha kuwa watu wa imani... “Enenda zako, imani yako imekuponya”. Tunapaswa kuomba neema ya Mungu ili tudumu katika imani. Tusichanganye imani ya Mungu na imani nyinginezo. Imani ya Bartimayo inahusisha utangazaji, sala, ukombozi, mkutano binafsi na kumfuasa Kristo. Ni kuzama ndani ya Yesu katika ibada, uchaji na utulivu wote… kuinua roho zetu na kuziweka mikononi mwa Mungu na kutumia muda wetu ndani yake na Yeye ndani yetu. Kusali si tu “maneno”. Kristo anaposikiliza maneno yetu “Mwalimu wangu, nataka nipate kuona” anatazama zaidi moyoni, anapima imani yetu kisha anaturuhusu “Enenda zako, imani yako imekuponya”, tudumu basi katika imani.

Waamini wote wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo vya imani na matumaini
Waamini wote wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo vya imani na matumaini

Bartimayo alilijua hitaji lake ni kuona! Je, tunatambua hasa hitaji la moyo wetu? Tukisikia Kristo anapita tutamuomba nini? Tusali ili tujaliwe macho ya rohoni tutambue lililo jema, macho maangavu kutambua shida za wenzetu, yaonayo ubaya wa nafsi zetu, yanayomulika ubinafsi ndani mwetu, yanayoskani tabia na mazoea yasiyofaa, tutupe majoho yetu ya udhaifu, tumkimbilie Kristo Mponyaji wetu. Bartimayo anawakilisha wote wanaopokea kwa moyo wote mwanga wa Kristo na sasa wanapata wokovu dhidi ya shetani, mateso ya mwili na mauti. Hii inahusisha Sakramenti ya Kitubio tunapoponywa upofu wetu wa dhambi.  Tuungame vema tukiweka pia nia/malengo madhubuti ya kuongoka, haifai kuungama bila kutoka katika mazingira ya dhambi. “Jipe moyo, inuka anakuita” ni maneno yenye matumaini ya kuponywa kutoka upofu wetu aina aina. Ulimwengu unatupofusha macho kwa kuleta upinzani, vitisho, ugumu wa maisha na majaribu. Tujipe moyo kwa kuwa katika Kristo yote ni nuru. Je, upofu wako ni upi? Tuombe neema ili kila mmoja atambue upofu wake wa kiroho, tutupe majoho yetu ya dhambi, tukiruka na kumkimbilia Kristo, tujitupe magotini pake, tuguswe na mkono wake wa uponyaji tukaishi vema na kuurithi uzima wa milele.

Liturujia D 30
26 October 2024, 09:02