蜜桃交友

Tafuta

Ni katika sala zake za kila siku alipokuwa na umri wa miaka 26, Paulo aligundua wazi kwamba Mungu alikuwa akimualika kuanzisha shirika ambalo lingeishi maisha na tunu za kiinjili ili kueneza kwa maneno na matendo upendo wa Mungu. Ni katika sala zake za kila siku alipokuwa na umri wa miaka 26, Paulo aligundua wazi kwamba Mungu alikuwa akimualika kuanzisha shirika ambalo lingeishi maisha na tunu za kiinjili ili kueneza kwa maneno na matendo upendo wa Mungu.  (ANSA)

Mtakatifu Paulo wa Msalaba: Uthubutu ni Zao la Imani Inayochagizwa na Utii

Mtakatifu Paulo alikuwa sio tu ni mwalimu wa sala lakini pia mtu wa sala ndio maana alifundisha kwamba “mtu anaye dharau sala ana chagua njia pana zaidi ya kuangamia.” Ni katika sala zake za kila siku alipokuwa na umri wa miaka 26, Paulo aligundua wazi kwamba Mungu alikuwa akimwalika kuanzisha Shirika ambalo lingeishi maisha na tunu za kiinjili ili kueneza kwa maneno na matendo upendo wa Mungu unaofunuliwa katika Mateso na Msalaba wa Kristo Yesu.

Na Padre Octavian Onesmo Hinju, Cp., - Morogoro, Tanzania.

UTANGULIZI: “Uthubutu ni ujasiri na nguvu ya ndani ya kufanya yale ambayo katika macho, fikra na mitazamo ya wengi hayawezekani. Uthubutu ni zao la imani kwa mwenyezi Mungu. Uthubutu unao chagizwa na utii kwa sauti ya Kristu, inayoendelea kusikika ndani mwetu ikisema ‘Duc in altum’ tweka mpaka kilindini, hutuvuta kufanya maamuzi sio kwa ajili yetu wenyewe bali kutimiza mpango wa Mungu kupitia sisi kwa ajili ya ukombozi wa watu wake. Ni Kurejelea tena na tena maneno ya Mwinjili Luka kwamba katika utayari wetu wa kutekeleza mpango wa huo “Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya” (Lk. 17:10) na kama Mama yetu Bikira Maria wa Msaada wa daima kwamba “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana. Na iwe kwangu kama ulivyosema.” (Lk. 1:38), ili kuweza kutembea na ‘Magnificat’ yaani utenzi wa shukrani kwa Mungu katika maisha yetu. Mpendwa Msikilizaji na Msomaji wa Pope, kila mwaka tarehe 19 Oktoba Mama Kanisa ulimwenguni kote anafanya kumbukumbu ya Mt. Paulo wa Msalaba Padre na Baba Mwanzilishi wa Shirika la kimisionari la Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristu. Paulo Francesco Danei alizaliwa huko Ovada, Piedmont katika miji ya Torino na Genoa nchini Italia mnamo tarehe 3 Januari mwaka1694 kwa baba Luca Danei na mama Anna Maria Massari. Ni mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watoto 16 wa baba na mama yake ambapo miongoni mwao ni 6 tu ndio walio salia kufuatia vifo wakati wa utoto, hii ilimfanya Paulo kuwa mkubwa kati ya watoto walio bakia. Kumbe katika muktadha huu, Paulo alijifunza tangu akiwa mdogo ukweli juu ya kifo na ugumu wa maisha. Hivyo kufanya maisha yake mwenyewe kuwa tafakari ya kwanza juu ya mateso na msalaba wa Kristu.

Mtakatifu Paulo wa Msalaba: Uthubutu ni zao la imani inayochagizwa na Utii.
Mtakatifu Paulo wa Msalaba: Uthubutu ni zao la imani inayochagizwa na Utii.

Kama ilivyo kwa watoto wengine, Paulo nae alipata elimu yake ya awali kutoka kwa Padre mlezi wa shule ya wavulana, huko Cremolino, Lombardi. Alipiga hatua na maendeleo makubwa lakini akiwa na umri wa miaka kumi na tano aliamua kuacha shule na kurudi nyumbani kwao Castellazzo; ambako alianza kufundisha katekesi katika makanisa na parokia za karibu. Akiwa na miaka 19 alijaliwa kwa mwangaza wa Roho Mtakatifu kupokea wongofu wa maisha ya sala mara baada ya kujisomea kwa undani maandishi ya Mt. Francisko wa Sale hasa kuhusu ‘Mafungo juu ya Upendo wa Mungu’; pamoja na maongozi ya kiroho kutoka kwa mapadre wa Shirika la Wafranciskani Wakapuchini, hivi vyote vikawa ni msingi wake kwa maisha yote ya kwamba Mungu anapatikana kwa urahisi zaidi katika Mateso ya Kristo. Mnamo 1715, Paulo alijiunga na jeshi ili kushiriki katika vita vya msalaba dhidi ya Waturuki lakini aligundua kuwa maisha ya uaskari sio wito wake. Paulo alikuwa sio tu ni mwalimu wa sala lakini pia mtu wa sala ndio maana alifundisha kwamba “mtu anaye dharau sala ana chagua njia pana zaidi ya kuangamia.” Ni katika sala zake za kila siku alipokuwa na umri wa miaka 26, Paulo aligundua wazi kwamba Mungu alikuwa akimualika kuanzisha shirika ambalo lingeishi maisha na tunu za kiinjili ili kueneza kwa maneno na matendo upendo wa Mungu unaofunuliwa katika Mateso na Msalaba wa Yesu Kristu.

Mtakatifu Paulo wa Msalaba Muasisi wa Shirika la Mateso
Mtakatifu Paulo wa Msalaba Muasisi wa Shirika la Mateso

Mapokeo na historia yanasimulia juu ya maono ya vazi la shirika lake ambalo yeye na wenzake wangevaa. Yaani kanzu nyeusi yenye alama ya moyo wa Yesu Mteseka yenye maneno JESU XPI PASSIO (Mateso ya Yesu Kristu) na mkanda mweusi wa ngozi kiunoni. Kwa mujibu wa kanuni ya mwanzo ya shirika, jina la kwanza ambalo Paulo alipendelea kwa ajili ya shirika lilikuwa ni ‘Maskini wa Yesu’; ambalo baadaye lilikuja kujulikana kama shirika la Mateso ya Yesu Kristo. Paulo aliandika kanuni ya shirika lake jipya wakati wa mafungo ya siku arobaini huko Castellazzo mwishoni mwa 1720. Akisaidwa na ndugu yake mwenyewe, Yohana Mbatizaji, Paulo alitaka shirika lije kuishi maisha ya toba, ukimya wa moyo na ufukara ili kuwafundisha watu kwa njia rahisi jinsi ya kutafakari Mateso ya Yesu. Ili kukidhi mahitaji ya kichungaji mara baada ya kozi fupi ya taalimungu, yeye pamoja na ndugu yake Yohana Mbatizaji walipewa daraja ya upadre na Baba Mtakatifu Benedikto XIII tarehe 7 Juni 1727, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Mjini Vatican. Baada ya kuwekwa wakfu walijitolea kuhubiri utume wa Kanisa katika parokia, hasa katika maeneo ya mashambani ambako hakukuwa na idadi ya kutosha ya mapadre walioshiriki katika uchungaji. Paulo alijulikana kuwa mmoja wa wahubiri maarufu zaidi wa siku zake, kwa maneno yake na kwa matendo yake ya huruma na ukarimu. Utume wao wa kuhubiri na mafungo waliyotoa katika seminari na nyumba za kitawa yaliusogeza utume wao kwa watu wengi na hatua kwa hatua shirika ilianza kukua.

Maisha yake yalisimikwa katika tafakari juu ya mateso na Msalaba wa Kristo.
Maisha yake yalisimikwa katika tafakari juu ya mateso na Msalaba wa Kristo.

Mtakatifu Paulo wa Msalaba aliandika zaidi ya barua elfu mbili, nyingi zikiwa ni barua za mwongozo wa maisha ya kiroho ambazo zimehifadhiwa huko makao makuu ya shirika jijini Roma Italia. Miaka michache kabla ya kifo chake alianzisha pia monasteri ya watawa wakaa pweke huko Corneto inayojulikana leo kama Tarquinia, ili kukuza kumbukumbu ya Mateso ya Yesu kwa maisha yao ya sala, toba na wongofu wa ndani. Alifariki dunia tarehe 18 Oktoba 1775, kwenye nyumba kuu ya Watakatifu Yohana na Paulo yalipo makao makuu ya shirika duniani. Paulo wa Msalaba alitangazwa kuwa Mwenyeheri tarehe 1 Oktoba 1852, na kutangazwa kuwa Mtakatifu tarehe 29 Juni 1867 na Papa Pio wa IX. Miaka miwili baadaye, sikukuu yake iliwekwa katika kalenda ya Kanisa na kuanza kuadhimishwa tarehe 19 Oktoba, siku baada ya siku ya kifo chake, kwani tarehe 18 Oktoba ni sikukuu ya Mwinjili Luka. Hata leo shirika limekuwa na kuenea ulimwengu mzima likijitahidi kushika na kuiishi kiaminifu karama ya mwanzilishi yaani “kuweka hai kumbukumbu ya mateso ya Yesu yaani “memoria passionis.” Kwa kutambua kuwa karama ni zawadi toka kwa Mungu na ni tunda la imani, Shirika linakuwa na kuendelea kushiriki mateso ya Kristu pamoja na wasulubiwa wa nyakati hizi kwa namna ya maisha ya kitume na huduma kwa maskini. Kumbe, katika hali ya ukimya tumwombe Kristu aseme nasi juu ya kile ambacho kila mmoja wetu anaitwa kukitangaza kwa Mataifa yote. Hata sasa Tumeendelea kuwashuhudia vijana wengi kote ulimwenguni wakijiweka wakfu kwa Mungu kupitia shirika hili ili kuendeleza kazi hii njema ya kuwa kumbusha watu kuwa “mateso ya Kristu ni kazi kuu na ya ajabu sana ya upendo wa Mungu” kama anavyosema Mtakatifu Paulo mwenyewe kwamba “Msalaba ni njia pekee ya kuelekea paradiso lakini ni endapo tu mtu ataubeba kwa hiari na moyo radhi.” Kwa njia ya sala na tafakari ya Neno la Mungu, tunatambua kwamba “msalaba ni utukufu wa Kristo na ushindi. Tunapokuwa na nguvu au kuanguka msalaba hutuinua. Msalaba ni hazina kubwa na ya thamani. Anayepata tuzo ya msalaba anapata hazina kuu, anasema Mt. Andrea wa Kreti.

Mtakatifu Paulo wa Msalaba: Tangazeni huruma msamaha wa Mungu.
Mtakatifu Paulo wa Msalaba: Tangazeni huruma msamaha wa Mungu.

Paulo wa Msalaba ni Mtakatifu aliyejitoa sana kueneza mapendo makuu ya Mungu kwa wanadamu sio tu kwa watu wa kizazi chake bali kwa wakristu wabatizwa wa nyakati zote. Akinukuu maneno ya Mtume Paulo katika Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho unaosema kwamba “sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa Msalabani, ujumbe ambao ni kikwazo kwa Wayahudi, na kwa Wagiriki ni upuuzi. Lakini kwa walioitwa, Wayahudi kwa Wagiriki, Kristo ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. Kwa maana huu ‘ujinga’ wa Mungu una hekima zaidi kuliko hekima ya wanadamu, na ’udhaifu’ wa Mungu una nguvu ipitayo nguvu ya wanadamu (1 Kor. 1:23-25), Paulo alitaka wafuasi wake wa vizazi vingi vijavyo wajiandae kikamilifu na wawe tayari kujichukulia mwilini mwao chapa zake Yesu (Wagal. 6:17), yaani mateso yake yaletayo wokovu. Daima alifundisha na kukaza kusema kwamba “Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristu ni ishara ya upendo wa Mungu Baba kwa wanadamu. Katika Msalaba tunachota wema, huruma na msamaha; na “Msalaba ni kitovu cha ulimwengu na moyo wa mwanadamu, mahali pa utulivu na udumifu” kama anavyosema Kardinali Robert Sarah kutoka Conakry Guinea kwenye kitabu chake maarufu kiitwacho “God or Nothing.” Kumbe, Msalaba ni kilele cha upendo wa Mungu kwetu na Kalvari panakuwa kwetu sio tena sehemu ya kifo, mauti na aibu bali mahali pa kuanza upya kwa imani, mapendo na matumaini makubwa. Kifo cha Yesu Msalabani ni mwanzo wa uhai na uzima mpya, uzima wa milele, anaendelea kusema Kardinali Robert Sarah.

Msalaba wa Kristo Yesu ni chemchemi ya uadilifu na utakatifu wa maisha
Msalaba wa Kristo Yesu ni chemchemi ya uadilifu na utakatifu wa maisha

Miaka 300 baada ya kuanzishwa kwa shirika bado roho ya uthubutu aliyokuwa nayo Mt. Paulo ni endelevu miongoni mwa wanachama na katika shirika zima. Itakumbukwa kuwa Paulo alithubutu kwa imani kuitii sauti iliyo mkataza asiwe mwanajeshi na hata ile iliyo msukuma kuanzisha taasisi kwa Sakramenti ya ndoa takatifu. Aliyaacha hayo yote ili kutimiza mpango wa Mungu wa kuwa mtawa na kuanzisha shirika; lakini pia alikataliwa mara kadhaa alipotaka kumwona Baba Mtakatifu ili kuidhinishwa kwa kanuni ya kwanza ya shirika lake. Akiongozwa na maisha ya sala Paulo anatufundisha na sisi kwanza kuweka tumaini letu kwa Mungu katika hali na namna zote. Pili kujiweka tayari kukabiliana na changamoto za maisha kwa imani. Ndiko kuthubutu kuyafanya mema tukiamini ni Mungu mwenyewe ndiye atendaye ndani mwetu. Kwa mfano wa maisha na utayari wake Paulo anatukumbusha Imani ya baba yetu wa Abrahamu aliyethubutu kuacha nchi yake na jamaa zake, na kwenda nchi aliyo agizwa na Mungu akiamini kuwa Mungu yuko nyuma yake akimlinda “Mimi ni Mungu mwenye nguvu. Fuata mwongozo wangu na kuishi bila lawama. Nami nitafanya agano nawe na kuwazidisha wazawa wako.” (Mwz. 17: 1-2). Kumbe basi, “Uthubutu ni ujasiri na nguvu ya ndani ya kufanya yale ambayo katika macho, fikra mitazamo ya wengi hayawezekani. Uthubutu ni zao la imani kwa mwenyezi Mungu. Uthubutu unao chagizwa na utii kwa sauti ya Kristu, inayoendelea kusikika ndani mwetu ikisema ‘Duc in altum’ “tweka mpaka kilindini” hutuvuta kufanya maamuzi sio kwa ajili yetu wenyewe bali kutimiza mpango wa Mungu kupitia sisi kwa ajili ya ukombozi wa watu wake. Ni Kurejelea tena na tena maneno ya Mwinjili Luka kwamba katika utayari wetu wa kutekeleza mpango wa huo “Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya” (Lk. 17:10) na kama Mama yetu Bikira Maria wa Msaada wa daima kwamba “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana. Na iwe kwangu kama ulivyosema.” (Lk. 1:38), ili kuweza kutembea na ‘Magnificat’ yaani utenzi wa shukrani kwa Mungu katika maisha yetu.

Msalaba wa Kristo ni chemchemi ya maisha na uzima wa milele
Msalaba wa Kristo ni chemchemi ya maisha na uzima wa milele

Tunapoitazama jana kwa shukrani tuiishi leo kwa imani na furaha ili tuweze kuifikia kesho tukiwa bado na tumaini kuwa Mungu anaendelea kuita watu kwenye shirika na maisha ya wakfu. Roho ya uthubutu na utayari wa kitume itusukume sisi nasi kuwa wamisionari katika nchi na mazingira yetu wenyewe. Bila woga wowote shirika liwe tayari kufungua maeneo mapya ya utume kwa kuzingatia mahitaji ya watu wa Mungu na Kanisa mahalia. Tufahamu kuwa “utume tulio upokea unahusisha Msalaba mzito lakini Kristu atatujalia neema ya kuweza kuubeba”, kama anavyo kaza kusema Kardinal Robert Sarah.  Kama wakristu wabatizwa katika ulimwengu mamboleo unaoendelea kuzongwa na choyo na ubinafsi, chuki, uhasama na vita vya kutumia silaha kali za maangamizi na uchu wa madaraka; Mt. Paulo ni shule ya mapendo na ukarimu kwa jirani. Anatufundisha kuruhusu mioyo yetu iguswe moja kwa moja na mahitaji ya wengine na kuwa tayari kuyasadaka maisha yetu kwa ajili yao. Kwani huduma kwa maskini ni ushiriki wa wazi katika kazi njema ya uinjilishaji. Ni kumuiga na kushirikiana na Kristu katika kuwakomboa wanadamu. Tukisaidiwa na msaada wa sala na maombezi yake, sisi nasi tudumu waaminifu kwa wito wetu tuliopokea kama zawadi ya thamani toka kwa Mungu na tuthubutu kufanya yote kwa sifa na utukufu wa Mungu. MATESO YA BWANA WETU YESU KRISTU, YAWE DAIMA MIOYONI MWETU; Mt. Paulo wa Msalaba, utuombee.

28 October 2023, 10:00